EWURA CCC: ELIMU KWA WATUMIAJI NDIYO SILAHA YA KUPUMGUZA BILI NA KULINDA USALAAMA
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limesema elimu kwa watumiaji wa huduma za maji, umeme, mafuta na gesi ni njia muhimu ya kupunguza bili zisizo za lazima, kuimarisha usalama na kuhakikisha wananchi wanatambua haki na wajibu wao wanapotumia huduma hizo.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji Mwandamizi wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, amesema baraza hilo linatumia maonesho hayo kuwafikia wananchi kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za nishati na maji.
"Tunatoa elimu kwa wananchi ili wawe watumiaji wenye taarifa sahihi, kwa sababu mtumiaji anayefahamu haki na wajibu wake ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuepuka gharama zisizo za lazima," amesema Lugiko.
Ameongeza kuwa watumiaji wa umeme wanapaswa kutumia mafundi wenye leseni ya EWURA, kufunga vifaa vya viwango vinavyokubalika na kufanya ukaguzi wa miundombinu ya umeme mara kwa mara ili kupunguza matumizi makubwa ya umeme pamoja na kuepusha ajali.
Kwa upande wa huduma za maji, amesema wananchi wanapaswa kuhakiki usomaji wa mita na kuchunguza uwepo wa uvujaji wa maji kabla ya kulalamikia bili kubwa, huku akieleza kuwa changamoto nyingi husababishwa na hitilafu zinazoweza kuzuilika.
Aidha, amewataka watumiaji wa mafuta kuhakiki bei rasmi zinazotangazwa na EWURA, kuhakikisha pampu inaanzia sifuri wakati wa kujaza mafuta na kudai risiti kama ushahidi wa manunuzi, huku akisisitiza kuepuka kununua mafuta katika vituo visivyo na leseni.
Lugiko pia amewahimiza Watanzania kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme na gesi, akisema matumizi yake ni salama, yanaokoa muda na yanachangia kulinda mazingira pamoja na kuboresha afya za wananchi.





