UTT AMIS YAWAHAMASISHA WATANZANIA KUWEKEZA KUPITIA MIFUKO YA UWEKEZAJI WA PAMOJA
Watanzania wamehimizwa kutumia fursa za uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja ili kujenga akiba, kuongeza mitaji na kupata faida shindani, huku wakihakikishiwa urahisi wa kuwekeza na kutoa fedha kupitia mifumo ya kidijitali.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa UTT AMIS, Bi. Martha Mashiku, wakati akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Amesema UTT AMIS imekuwa ikitoa huduma za uwekezaji kwa takribani miaka 20 na kwa sasa inasimamia rasilimali zenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 5.3 pamoja na kuwa na zaidi ya wawekezaji 600,000.
Mashiku amesema taasisi hiyo hukusanya mitaji kutoka kwa watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali na kuiwekeza katika masoko ya fedha na mitaji ili kuzalisha faida kwa wawekezaji.
Ameeleza kuwa UTT AMIS imeboresha mifumo yake ya kidijitali, ambapo mwekezaji anaweza kufungua akaunti, kufuatilia miamala, kusasisha taarifa zake na kutoa fedha zisizozidi Sh milioni 5 kupitia simu ya mkononi bila kufika ofisini.
Kwa mujibu wake, fedha zinazotolewa hulipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya mwekezaji ndani ya siku tatu hadi 10 za kazi, kutegemeana na aina ya mfuko aliowekeza.
Amesema kwa wanaotaka kutoa zaidi ya Sh milioni 5, wanapaswa kufika katika ofisi za UTT AMIS au kujaza fomu kupitia tovuti ya taasisi hiyo kabla ya fedha zao kulipwa ndani ya muda uliowekwa.
Mashiku amesema baadhi ya mifuko ya uwekezaji hutoa gawio kwa wawekezaji, ikiwemo Mfuko wa Jikimu unaolipa gawio mara nne kwa mwaka kwa waliowekeza kuanzia Sh milioni 2, huku Mfuko wa Hatifungani ukitoa gawio kila mwezi kwa waliowekeza kuanzia Sh milioni 10.
Aidha, amesema uwekezaji unaweza kuanza kwa kiwango cha chini cha Sh 15,000, ambapo wananchi wanaweza kuongeza fedha kidogo kidogo kulingana na uwezo wao na kunufaika na faida ya muda mrefu kupitia mfumo wa faida jumuishi.
Mashiku amewaalika wananchi kutembelea banda la UTT AMIS lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Fedha katika maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu ya uwekezaji, kufungua akaunti na kuanza kuwekeza papo hapo kupitia benki au mitandao ya simu.
Amesisitiza kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji na kuimarisha ujumuishi wa kifedha kupitia huduma zinazopatikana kwa urahisi nchini kote.







