Breaking News

FUNDI SIMU ATOA ELIMU JINSI YA KUOKOTA DATA NA KUJILINDA DHIDI YA UTAPELI MTANDAONI

Wananchi wametakiwa kutumia kwa uangalifu simu za mkononi na huduma za intaneti ili kupunguza matumizi makubwa ya data pamoja na kujikinga dhidi ya utapeli unaofanyika kupitia mitandao ya kijamii.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Umoja wa Mafundi Simu Dar es Salaam na Pwani, Hussein Abdulrahman Suleiman, wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo mafundi simu wanatoa elimu kwa umma kupitia banda la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hussein alisema hatua ya kwanza kwa mtumiaji wa simu ni kuelewa namna kifaa chake kinavyotumia data, kwani programu nyingi huendelea kutumia intaneti hata pale mtumiaji anapokuwa haziendeshi.

Alisema watumiaji wanaweza kupunguza matumizi ya data kwa kuzima kipengele cha Background Data katika programu wanazotumia mara kwa mara.

"Mtumiaji anaweza kwenda kwenye sehemu ya Settings, akafungua Applications, achague programu husika kama WhatsApp au TikTok, kisha afungue sehemu ya Mobile Data na kuzima Background Data. Hii huzuia programu kutumia data bila ulazima, huku ikiendelea kufanya kazi kawaida pale inapofunguliwa," alisema.

Mbali na matumizi ya data, Hussein alitoa tahadhari kuhusu ongezeko la utapeli wa mtandaoni, akiwataka wananchi kuwa waangalifu wanapobofya viunganishi (links) vinavyotumwa kupitia mitandao ya kijamii au programu za mawasiliano.

Alisema baadhi ya viunganishi hivyo hutumiwa na wahalifu wa mtandaoni kudukua akaunti za watumiaji na kuiba taarifa zao binafsi.

Kwa upande wa mafundi simu, Hussein aliwataka kujisajili kupitia mfumo wa TCRA unaojulikana kama Tanzanite Portal, ili wapate leseni zinazowatambua rasmi na kuwawezesha kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Alisema usajili huo unarahisisha mafundi kupata msaada kutoka kwa mamlaka husika endapo watakumbana na changamoto katika shughuli zao za kila siku.

"Fundi simu aliyesajiliwa anatambulika na TCRA, jambo linalompa uhalali wa kufanya kazi na kurahisisha kushughulikiwa pale changamoto zinapotokea," alisema.

Pia aliwashauri wananchi kuwa makini wanaponunua simu mpya kwa kuhakikisha wanazingatia ubora wa kifaa badala ya bei pekee.

Alieleza kuwa baadhi ya simu zisizo na viwango bora hukosa uwezo wa kurekebisha mwanga wa skrini, hali inayoweza kuathiri afya ya macho ya mtumiaji.

Kwa mujibu wa Hussein, elimu inayotolewa katika Maonesho ya Sabasaba imeendelea kuwavutia wananchi wengi, huku ikiwasaidia kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya simu za mkononi na teknolojia za mawasiliano.