Breaking News

MIX YAITANGAZA SABASABA YA CASHLESS, YAWAHIMIZA WATANZANIA KUCHANGAMKIA MALIPO YA KIDIJITALI

Dar es Salaam. Kampuni ya Mix imesema Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameleta sura mpya ya matumizi ya teknolojia ya kidijitali, huku ikiyataja kuwa ni Sabasaba ya Cashless kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu.

Akizungumza leo Julai 3, 2026, katika viwanja vya Sabasaba, mwakilishi wa kampuni hiyo alisema Mix imejipanga kuhakikisha Watanzania wanatumia kikamilifu huduma za kidijitali katika kufanya malipo mbalimbali ndani ya maonesho hayo.

Alisema kupitia huduma ya Lipa kwa Simu ya Mix, wananchi wanaweza kufanya malipo ya kuingia maoneshoni na kununua bidhaa au huduma kwa urahisi bila kubeba fedha taslimu.

"Katika banda letu la Mix tumewawekea huduma zote muhimu. Wateja wanaweza kuweka fedha kwenye akaunti zao kupitia mawakala waliopo, kupata maelezo kuhusu huduma zetu mbalimbali, au kujiunga kuwa mawakala wa Mix papo hapo," alisema.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeendelea kuboresha Mix Super App kwa kuongeza huduma mbalimbali zinazorahisisha maisha ya kidijitali kwa wananchi.

Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda la Mix ili kujifunza matumizi ya huduma hizo na kupata fursa ya kuishi maisha ya kisasa yanayotegemea teknolojia ya kidijitali.

Akizungumzia kampeni ya Kombe la Dunia, alisema Mix imeanza kuwapeleka washindi kwenda kushuhudia mechi za Kombe la Dunia nchini Mexico, huku akibainisha kuwa kampeni hiyo bado inaendelea.

Alisema kila siku washiriki wana nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali zikiwemo Sh milioni 1.6, friji na spika, huku mshindi wa mwisho wa kampeni hiyo akitarajiwa kujishindia Sh milioni 50 mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania kutembelea banda la Mix katika Maonesho ya Sabasaba na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo, akisema zimeboreshwa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa huduma za kidijitali.

Pia aliwashukuru waandaaji wa maonesho kwa kuweka mazingira yanayochochea matumizi ya malipo ya kidijitali, akisema hatua hiyo inaendana na mwelekeo wa dunia wa uchumi wa kidijitali.