Breaking News

NCHIMBI: TANZANIA ITAENDELEA KUIUNGA MKONO OACPS KATIKA MAGEUZI

Na Mwandishi Wetu, Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameihakikishia Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuimarisha mageuzi na kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo kwa manufaa ya nchi wanachama.

Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Julai 26, 2026, jijini Arusha alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa OACPS, Moussa Saleh Batraki.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alimpongeza Katibu Mkuu wa OACPS kwa hatua anazochukua katika kutekeleza ajenda ya mageuzi, ikiwemo kuimarisha uadilifu na kupunguza utegemezi, hatua zinazolenga kuifanya jumuiya hiyo kuwa imara na yenye tija zaidi kwa wanachama wake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OACPS alisema taasisi hiyo imejipanga kuweka mkazo katika kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama, pamoja na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, alisema OACPS itaendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji katika sekta ya TEHAMA, hususan teknolojia za kidijitali, akili unde, ulinzi na usimamizi wa takwimu na taarifa, sambamba na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi zinazoendelea na kuwajengea uwezo wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya, Jestas Nyamanga, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ellen Maduhu.