Breaking News

TLS, LHRC NA DKT. SLAA WAFUNGUA KESI MAHAKAMA KUU KUPINGA MARUFUKU YA MIKUTANO YA KISIASA


Dar Es Salaam: Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwanasiasa mkongwe Dkt. Wilbroad Slaa wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wakipinga agizo la Serikali la kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Akizungumza kwa niaba ya walalamikaji, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, amesema shauri hilo lenye namba 18/2026 linaomba Mahakama itangaze kuwa agizo hilo linakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji ni TLS kama mlalamikaji wa kwanza, LHRC kama mlalamikaji wa pili na Dkt. Wilbroad Slaa kama mlalamikaji wa tatu, ambaye amefungua shauri hilo kwa nafasi yake ya mwananchi kwa maslahi ya umma.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), pamoja na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, ikiwemo CHADEMA na ACT-Wazalendo, ambavyo vimejumuishwa katika shauri hilo kwa kuwa vinatajwa kuwa miongoni mwa wadau walioathiriwa na marufuku hiyo.

Walalamikaji wanadai kuwa marufuku hiyo inakiuka haki ya usawa mbele ya sheria kwa madai kwamba inawabagua wadau wa vyama vya upinzani, huku viongozi wa Serikali na chama tawala wakiendelea kufanya mikutano ya hadhara.

Aidha, wanasema agizo hilo linakiuka haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 18 na 20 za Katiba, pamoja na haki ya wananchi kushiriki katika shughuli za umma kwa mujibu wa Ibara ya 21.

Katika hoja nyingine, walalamikaji wanadai Waziri wa Mambo ya Ndani hana mamlaka ya kisheria ya kutoa marufuku ya jumla ya mikutano ya kisiasa nchini. Pia wanasisitiza kuwa Jeshi la Polisi haliwezi kuzuia mkutano wa kisiasa kabla ya kupokea taarifa rasmi kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia uamuzi wake wa kushiriki katika shauri hilo, Dkt. Wilbroad Slaa amesema ameamua kufungua kesi hiyo kama mwananchi anayelenga kulinda misingi ya Katiba, demokrasia na utawala wa sheria.

Amesema ni muhimu Tanzania iendelee kuheshimu haki za kikatiba za wananchi na kulinda uhuru wa kisiasa kwa mujibu wa sheria.

Shauri hilo kwa sasa linasubiri kupangiwa tarehe ya kutajwa na kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.