PPAA YATUMIA MFUKO WA KIDIJITALI KUHARAKISHA USULUHISHI WA RUFAA ZA ZABUNI
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema matumizi ya mfumo wa kidijitali wa NeST yameongeza kasi na uwazi katika kushughulikia malalamiko na rufaa za zabuni, hatua inayoimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkuu wa Sehemu ya Sheria wa PPAA, Agnes Sayi, kwa niaba ya Katibu Mtendaji James Sando, alisema mfumo huo ulioanza kutumika Februari 2025 umewezesha taasisi kushughulikia rufaa 58 kati ya 60 zilizowasilishwa katika mwaka wa fedha 2025/26, huku rufaa mbili zilizobaki zikiendelea kufanyiwa kazi katika mwaka huu wa fedha.
Sayi alisema moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya PPAA na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ikiwa na lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa huduma kwa wadau wa ununuzi wa umma.
Ameeleza kuwa hadi sasa wadau 2,600 wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo, wakiwemo wazabuni 1,907 pamoja na watumishi wa umma 705, hatua inayotarajiwa kuongeza matumizi sahihi ya huduma za kidijitali katika sekta ya ununuzi wa umma.
Aidha, alisema PPAA inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu namna ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa njia ya mfumo wa NeST ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Alibainisha kuwa matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa rufaa yanasaidia kujenga mazingira ya ushindani wa haki, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Serikali inapata thamani halisi ya fedha katika miradi ya umma.




