Breaking News

TASAC YAHIMIZWA KUIMARISHA ULINZI WA UWEKEZAJI NA KUZALISHA WATAALAM WA SEKTA YA BAHARIi

Serikali imeihakikishia sekta ya usafiri wa majini kuwa itaendelea kulinda uwekezaji wa vyombo vya majini pamoja na mali za wawekezaji ili kuweka mazingira salama ya biashara, huku ikiitaka Tanzania Shipping Agencies Corporation (TASAC) kuimarisha usimamizi na kuchochea upatikanaji wa wataalamu wa kutosha katika sekta hiyo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Maonesho ya 50 ya biashara (Sabasaba), Naibu waziri Uchukuzi David Kihenzile amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wawekezaji wanaowekeza katika meli, boti na vyombo vingine vya majini wanaendelea kufanya shughuli zao bila hofu, huku ulinzi wa raia, wasiokuwa raia na mali zao ukipewa kipaumbele kupitia taasisi husika za Serikali.

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza imani ya wawekezaji na kuvutia uwekezaji zaidi katika uchumi wa buluu, ambao unaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na ajira kwa Watanzania.
Aidha, alieleza kuwa ukuaji mkubwa wa biashara katika bandari za Tanzania unaonyesha mahitaji ya wataalamu wa sekta ya bahari yanaongezeka kwa kasi huku akifafanua kuwa kiwango cha mizigo kilichokuwa kinatarajiwa kufikiwa mwaka 2030 kilifikiwa mapema mwaka 2022 kutokana na uongozi madhubuti, kuimarika kwa diplomasia ya uchumi na ushiriki wa sekta binafsi.

Aidha Kihenzile amesema kuwa, ongezeko hilo la mizigo linamaanisha kuwa kutahitajika manahodha, wasaidizi wa mabaharia na wataalamu wengine wengi zaidi ili kuhudumia shughuli zinazopanuka katika sekta ya usafiri wa majini.

Kutokana na hali hiyo, Kihenzile ameitaka TASAC kutotekeleza jukumu la udhibiti pekee, bali kushirikiana na Serikali kuweka mikakati ya kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaokidhi mahitaji ya sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Pia amewapongeza watumishi wa TASAC kwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi, akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo ili kuhakikisha manufaa ya sekta ya bahari yanawanufaisha Watanzania wote na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.