Breaking News

BUNGE LAITAKA SERIKALI KUONGEZA UWEKEZAJI TTCL

DAR ES SALAAM – Serikali imeshauriwa kuongeza uwekezaji na bajeti kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili kuongeza kasi ya upanuzi wa huduma za intaneti ya mkongo wa nyuzi (FTTH) na kuongeza mapato ya taifa.

Ushauri huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mhe, Abubakar Asenga wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Fiber Mlangoni Kwako unaotekelezwa na TTCL.

Asenga amesema Kamati ya Bunge ya Miundombinu itaendelea kujenga hoja ndani ya kamati na Bunge ili Serikali iongeze fedha na bajeti kwa TTCL, akieleza kuwa uwekezaji huo unaweza kuleta manufaa makubwa kwa taifa.
Amesema hadi mwaka wa fedha 2024/2025, TTCL imeweza kukusanya takribani Sh bilioni 100 kutokana na kuwaunganisha zaidi ya watu 280,000 na huduma hiyo, huku lengo likiwa kukusanya Sh bilioni 400 ifikapo mwaka 2029 kupitia kuwaunganisha watumiaji milioni moja.

“Kwa tukija kuunganisha watu milioni mbili, tutaweza kupata karibu trilioni moja kufikia mwaka 2030. Kwa nini Serikali isiwekeze zaidi?” amesema Asenga.

Kwa mujibu wa Asenga, matokeo hayo yanaonesha umuhimu wa Serikali kuendelea kuiwezesha TTCL ili shirika hilo liweze kuongeza wigo wa huduma na mapato yatokanayo na uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano.

Amesema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imekuwa ikishauri kwa miaka kadhaa kuhusu umuhimu wa kuipa TTCL nafasi kubwa katika usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano, hatua ambayo sasa inaanza kuonesha matokeo.
“Leo tunapata matunda ya kamati na ushauri wa miaka mitatu, minne nyuma kwamba mchongo wa Taifa umilikishwe TTCL. Yote yaliyosemwa hapa yanadhihirisha kwamba kamati ilisoma vizuri na Bunge lilishauri vizuri,” amesema.

Aidha, Asenga amesema Bunge lina wajibu wa kuisimamia na kuishauri Serikali pamoja na kuhakikisha maamuzi na ushauri unaotolewa unatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Amesema uwepo wa Kamati ya Miundombinu katika hafla hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la Bunge la kufuatilia kazi zinazofanywa na Serikali, huku akimpongeza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zilizofikiwa katika kuendeleza sekta ya mawasiliano.