FIBER MLANGONI KWAKO NI CHACHU YA UCHUMI WA KIDIJITALI
DAR ES SALAAM – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema utekelezaji wa mradi wa Fiber Mlangoni Kwako awamu ya pili ni hatua muhimu katika kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Fatuma Kalovya, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Mohammed Hamisi Abdulla, wakati wa hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.
Kalovya amesema mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, hususan intaneti yenye kasi, uhakika na inayopatikana kwa urahisi, huku ukichochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu imara ya mawasiliano katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa kuwa huduma za intaneti zinazopatikana kwa uhakika zinawezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kuongeza ufanisi wa shughuli zao.
“Mradi huu ni wa kimkakati na unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, hususan huduma ya intaneti ya kasi na ya uhakika, sambamba na kuchochea matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” amesema Kalovya.
Ameongeza kuwa mradi huo unaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, hususan matarajio ya kuhakikisha upatikanaji wa intaneti ya kasi na huduma za mawasiliano zilizo na uhakika na gharama nafuu kote nchini.
Kalovya amesema Wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma za mawasiliano na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo.
Aidha, amesema Wizara itaendelea kuisimamia TTCL katika utekelezaji wa mradi huo ili ufanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA na shughuli za kidijitali.
Awamu ya pili ya mradi wa Fiber Mlangoni Kwako inatarajiwa kutekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.




