CHALAMILA ATOA WIKI MOJA KUPATIWA UFUMBUZI MGOGORO WA ARDHI TOANGOMA
DAR ES SALAAM — Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa muda wa wiki moja kukutana na uongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na wadau wengine ili kutafuta muafaka wa mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi wa Toangoma, Wilaya ya Temeke, na shirika hilo.
Chalamila ametoa agizo hilo baada ya kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo na kusikiliza malalamiko yao pamoja na maelezo kutoka NSSF na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi kuhusu umiliki wa eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Toangoma, Chalamila amesema baada ya kusikiliza pande zote amejiridhisha kuwa eneo linalozungumziwa ni mali ya NSSF.
Hata hivyo, amesema amepokea ombi la wananchi la kutaka NSSF iwapunguzie gharama za ununuzi wa ardhi hiyo kutoka Sh15,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Malela na Sh 25,000 kwa mita ya mraba katika eneo la Mwapemba hadi Sh 5,000 kwa mita ya mraba.
Wananchi pia wameomba kuongezewa muda wa kulipia ardhi hiyo kutokana na hali zao za kiuchumi, ambapo NSSF awali iliwapa muda wa miezi mitatu.
“Katika kipindi hiki cha siku saba wananchi wasisumbuliwe. Nitakutana na wadau wote wanaohusika ili tupate muafaka wa suala hili,” amesema Chalamila.
Amesema baada ya kumalizika kwa muda huo wa wiki moja atarudi kufanya mkutano mwingine kwa lengo la kuhitimisha suala hilo, huku akieleza kuwa muda wa awali uliotolewa na NSSF kwa wananchi umesitishwa ili kuwezesha kutafutwa kwa mpango mpya.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Mwinuka, amethibitisha kuwa eneo hilo ni mali ya NSSF.
Naye Meneja Miliki kutoka NSSF amesema baada ya shirika kubaini kuwa eneo lake limevamiwa, liliamua kuwaingiza wananchi katika utaratibu wa kununua ardhi hiyo kwa bei ya Sh15,000 kwa mita ya mraba kwa eneo la Malela na Sh 25,000 kwa mita ya mraba kwa eneo la Mwapemba.
Awali, wananchi wa Toangoma walimwomba Chalamila kuingilia kati suala hilo na kuhakikisha NSSF inawauzia ardhi hiyo kwa gharama nafuu ya Sh 5,000 kwa mita ya mraba, wakieleza kuwa waliingia katika maeneo hayo kupitia taratibu walizoelekezwa na uongozi wa serikali za mitaa.
Aidha, wananchi hao waliomba kuongezewa muda wa kulipia ardhi hiyo kutoka miezi mitatu hadi kati ya miaka minne na 10, wakieleza kuwa kipato chao hakiwaruhusu kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika eneo hilo, wananchi wengi walianza kuingia katika maeneo hayo zaidi ya miaka 16 iliyopita baada ya kuuziwa ardhi kupitia ofisi za serikali za mitaa, huku wakiamini kuwa maeneo hayo hayakuwa chini ya umiliki wa NSSF.
Mgogoro huo umeendelea kwa muda mrefu, huku wananchi wakitaka suluhisho litakalowawezesha kubaki katika maeneo hayo kwa masharti wanayoweza kuyamudu, wakati NSSF ikisisitiza umiliki wake wa kisheria wa eneo hilo.






