ITALIA YAVUTIWA NA MFUMO WA TANZANIA WA KUTOA ELIMU YA ZIMAMOTO
Dodoma - WADAU kutoka Italia wameeleza kuvutiwa na mfumo unaotumiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania wa kuwafikishia wananchi moja kwa moja elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga, wakisema utaratibu huo unaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine.
Wadau hao walitoa kauli hiyo baada ya kutembelea Banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2026, yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Wakati wa ziara hiyo, walipata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi hilo, hususan katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia moto na kuchukua tahadhari dhidi ya majanga.
Mmoja wa wadau hao kutoka Italia alisema aliguswa zaidi na namna Jeshi hilo linavyowafikia wananchi katika mazingira yao ya kawaida na kuwapa fursa ya kukutana moja kwa moja na wataalamu wa Zimamoto na Uokoaji.
Alisema utaratibu huo unatofautiana na ule unaotumika kwa kiasi kikubwa nchini Italia, ambako elimu ya aina hiyo hutolewa zaidi kupitia taasisi maalum za elimu, ikiwemo shule na vyuo.
“Nimevutiwa sana na namna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania linavyowafikia wananchi moja kwa moja na kuwapa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga. Kwetu Italia, mara nyingi elimu kama hii hupatikana kupitia taasisi maalum kama shule na vyuo. Tanzania inafanya jambo zuri kwa kuifikisha elimu hii moja kwa moja kwa jamii,” alisema.
Elimu inayotolewa inahusu matumizi salama ya nishati na vifaa vya umeme, matumizi sahihi ya vizima moto, namna ya kutoa taarifa za dharura pamoja na hatua za awali za kuchukua pindi janga linapotokea.
Ushiriki wa Jeshi hilo katika maonesho hayo umeifanya Nanenane kuwa fursa kwa wananchi kupata elimu ya vitendo kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya majanga, huku ukiendelea kuimarisha dhana kwamba kinga ni jukumu la kila mmoja na tahadhari ya mapema ni msingi wa kupunguza madhara ya majanga.










