Breaking News

MAMBO COFFEE YATANGAZA FURSA ZA SOKO LA NDANI NA NJE KWA WAKULIMA WA KAHAWA

DODOMA: Kampuni ya Mambo Coffee Company Limited imesema imejipanga kuongeza thamani ya zao la kahawa kwa kusindika na kuuza kahawa katika soko la ndani na nje ya nchi, huku ikiwahamasisha wakulima na wadau wa sekta hiyo kutumia fursa za ushirikiano ili kuongeza tija na kipato.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mtaalamu wa Maabara ya Kahawa na Mkaangaji wa Kahawa (Lab Technician na Roaster), Jamal Kasim Kisoma, alisema kampuni hiyo huuza kahawa ghafi (green coffee) katika masoko ya kimataifa kwa wateja wanaojiandalia uchakataji wao, sambamba na kuuza kahawa iliyokaangwa kwa soko la ndani.

Alisema Mambo Coffee hutumia kiwango cha Medium Roast, ambacho huifanya kahawa kuhifadhi ladha, harufu na ubora wake kwa kiwango kinachokubalika na walaji wengi.

"Kahawa yetu huokaangwa kwa kiwango cha kati ili kuhifadhi ladha halisi, harufu nzuri na virutubisho vinavyopatikana kwenye kahawa, hivyo kuwapatia wateja bidhaa yenye ubora wa hali ya juu," alisema.

Aidha, alisema kampuni hiyo hutoa bidhaa mbalimbali zikiwemo kahawa ya punje zilizokaangwa (roasted beans) kwa hoteli, migahawa na ofisi, pamoja na kahawa iliyosagwa kwa matumizi ya taasisi na biashara mbalimbali.

Pia alibainisha kuwa Mambo Coffee hushirikiana na vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima kwa kununua kahawa yao, hatua inayochangia kuongeza uzalishaji, kuboresha masoko na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati baada ya mauzo ya mazao yao.