Breaking News

JOWUTA KUPATA UGENI WA WAANDISHI WA HABARI OMAN, KUJADILI USHIRIKIANO

Na Mwandishi Wetu - Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kesho kinatarajia kupokea ugeni kutoka Chama cha Waandishi wa Habari cha Oman (Omani Journalists Association - OJA), unaotarajiwa kuwasili nchini leo, Jumanne, Agosti 18, 2026. 

Taarifa ya ujio wa ugeni huo imetolewa na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya ambaye amesema wameuchukulia kwa uzito ugeni huo kutoka Oman.

"Ugeni huo unakuja nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na JOWUTA katika nyanja mbalimbali, ikiwemo eneo la kitaaluma," alisem.

Msuya alisema ugeni huo wa wajumbe wanne kutoka Oman utakutana na viongozi wa JOWUTA, ambapo mazungumzo yatajikita katika kuandaa kongamano litakalojulikana kama Oman – Tanzania Journalists Forum.

Pia alisema viongozi watajadiliana kuhusu ushirikiano baina ya JOWUTA na OJA, Programu za kubadilishana uzoefu baina ya waandishi wa habari wa Tanzania na Oman.

Katibu Mkuu alisema ugeni huo unatarajiwa kukutana na viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Maliasili na Utalii, kabla ya kwenda Zanzibar baadaye.