Breaking News

JWTZ MWENYEJI WA MAADHIMISHO YA SITA YA WIKI YA USHIRIKIANO WA MAJESHI YA EAC 2026

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajiwa kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Ushirikiano wa Majeshi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yatakayoanza tarehe 26 Agosti hadi tarehe 1 Septemba 2026 hapa nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Jeshini, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua ameeleza kuwa maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, ambapo mara ya mwisho kufanyika nchini Tanzania ilikuwa mwaka 2022.

Katika kuadhimisha wiki hiyo, Majeshi hayo yatatoa huduma mbalimbali za kijamii na misaada ya kibinadamu kwa wananchi. Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na matibabu ya bure yatakayotolewa na madaktari bingwa kutoka nchi za Burundi, Somalia, Tanzania, Rwanda, Kenya, na Uganda.

Aidha, maadhimisho hayo yatahusisha shughuli za ukarabati na utoaji wa misaada ya kijamii katika vituo vya afya, vituo vya kulelea watoto yatima, na Magereza katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, na Zanzibar.

Baadhi ya vituo vitakavyonufaika na huduma na ukarabati huo ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Hospitali ya Vijibweni Kigamboni, na Kituo cha Afya Yombo Malawi (Dar es Salaam), Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi na Hospitali ya Wilaya Bagamoyo (Pwani), pamoja na Hospitali za Wilaya za Mwerapongwe Unguja na Vitongoji Pemba.

Vilevile, misaada hiyo itawafikia wafungwa katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam na Gereza la Kisongo Mkoani Arusha, sambamba na vituo vya kulelea watoto yatima vya Kurasini, Mwandaiwa Orphanage Centre Bunju, Chanika Children Shelter (Dar es Salaam), SOS Orphanage Centre Zanzibar, na vituo vya afya vya Kibokoni Pemba na Mapinduzi Dodoma - Chamwino