KAMPENI ZA UPOTOSHAJI MITANDAONI ZAZIDI KUKOSA MASHIKO UWEKEZAJI MKUBWA KOROSHO WAJA
Tanzania inazidi kutakata na kimataifa katika kuvutia mitaji mikubwa ya kigeni, huku juhudi za baadhi ya watu wanaojaribu kuzuia maendeleo na uwekezaji nchini kupitia maneno ya ovyo na kampeni za upotoshaji mitandaoni zikizidi kukosa mashiko.
Wakati wapinga maendeleo wakijitahidi kupotosha ukweli mtandaoni, vitendo na ukweli wa uwekezaji thabiti kutoka kwa wawekezaji wakubwa wa kimataifa unazidi kudhihirisha ustawi wa nchi, ukiwemo uamuzi wa kimkakati wa Kampuni ya ubanguaji wa korosho ya Sarl Anacard'Or kutoka Algeria kujenga viwanda vitatu vya kisasa nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho na kuliteka soko la dunia.
Mpango huo mkubwa wa uwekezaji uliothibitishwa na Mmiliki na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Walid Dib, utaanza rasmi kwa ujenzi wa kiwanda cha kisasa kabisa wilayani Masasi mkoani Mtwara, kitakachofungwa mashine za kisasa kutoka Vietnam ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa wa kiwango cha juu.
Akizungumza wakati wa ziara ya Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, katika kiwanda cha kampuni hiyo jijini Oran, Dib alieleza wazi kuwa wamevutiwa mno na ubora wa kipekee wa korosho ya Tanzania, jambo lililowafanya waamue kununua korosho za Tanzania pekee na kuongeza mtaji wao nchini humo huku makontena kadhaa yakiwa tayari yameshapokewa na mengine yakiwa safarini kuelekea Algeria.
Kwa upande wake, Balozi Matinyi alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha na mazingira rafiki kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, jambo ambalo litaleta tija kubwa ikiwemo kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza mapato ya serikali, kuhamisha teknolojia na ujuzi, pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
Ushahidi huu wa wazi wa uwekezaji wa kimataifa unazima kabisa kelele za mitandaoni na kuthibitisha kuwa Tanzania inazidi kupiga hatua kubwa kiuchumi chini ya misingi bora ya uwekezaji inayovuta makampuni makubwa duniani.




