MATUMIZI YA HUDUMA ZA MAWASILIANO YAONGEZEKA NCHINI
Dar es Salaam - MATUMIZI ya huduma za mawasiliano nchini yameendelea kuongezeka katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026, huku usajili wa laini za simu ukifikia milioni 116.95 na usajili wa intaneti kufikia milioni 62.79.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, amesema ongezeko hilo linaonesha namna mawasiliano yanavyozidi kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo biashara, elimu, huduma za kifedha, ajira na upatikanaji wa taarifa.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya hali ya sekta ya mawasiliano kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/26, Kairuki alisema takwimu hizo zinaonesha kuwa matumizi ya huduma za simu, intaneti, utangazaji, posta na usafirishaji wa vifurushi yanaendelea kukua.
“Sekta ya mawasiliano imeendelea kukua na kuwa sehemu muhimu sana ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini,” alisema.
Alisema huduma za simu na intaneti kwa sasa hazitumiki tena kwa mawasiliano pekee, bali zimekuwa miundombinu muhimu inayowezesha biashara, elimu, huduma za kifedha, ajira, upatikanaji wa taarifa na huduma mbalimbali za kijamii.
Intaneti, data yaongezeka
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, usajili wa intaneti uliongezeka kwa asilimia 6 hadi kufikia laini milioni 62.79 Juni 2026, kutoka milioni 58.97 zilizorekodiwa Machi mwaka huo.
Matumizi ya data nayo yaliongezeka kwa asilimia 11 katika kipindi hicho, hali ambayo imehusishwa na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, video, elimu mtandaoni, biashara, huduma za kifedha na huduma nyingine za kidijitali.
Waziri alisema ongezeko hilo linaonesha mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika maisha ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata vifaa vinavyowezesha matumizi ya huduma za kisasa za intaneti.
Simu janja zafikia asilimia 44.8
Takwimu hizo zinaonesha kuwa matumizi ya simu janja yameongezeka kutoka asilimia 42.5 Machi 2026 hadi asilimia 44.8 Juni mwaka huo.
Kairuki alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa kuwa simu janja zinawawezesha wananchi kutumia programu na huduma mbalimbali za kidijitali.
Alitoa mfano wa wakulima ambao, kupitia simu janja, wanaweza kupata taarifa za hali ya hewa, kujifunza mbinu za kisasa za kilimo, kutambua changamoto za mazao, kupata masoko na kufanya malipo ya kidijitali.
Hata hivyo, alisema bado kuna kazi ya kuongeza idadi ya wananchi wenye simu janja pamoja na kuwajengea ujuzi wa kuzitumia ipasavyo.
Huduma za pesa mtandao zaongezeka
Akaunti za huduma za pesa mtandao ziliongezeka kwa asilimia 7.5 kutoka milioni 80.97 Machi 2026 hadi milioni 87.47 Juni mwaka huo.
Kairuki alisema ongezeko hilo linaonesha kuwa wananchi wanazidi kutumia huduma za kidijitali katika kupokea na kutuma fedha, kulipia bidhaa na huduma, kufanya biashara pamoja na malipo mbalimbali.
Alisema kwa sasa wananchi wanaweza kufanya shughuli nyingi za kifedha kupitia simu bila kutegemea matumizi ya fedha taslimu.
Utapeli wa simu wapungua
Kwa upande mwingine, matukio ya ulaghai na utapeli kupitia simu yalipungua kwa asilimia 25.9, kutoka matukio 9,816 katika robo iliyoishia Machi 2026 hadi 7,334 Juni mwaka huo.
Hata hivyo, baadhi ya mikoa imeendelea kuwa na idadi kubwa ya matukio hayo, huku Rukwa na Morogoro ikitajwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuendelea kupewa elimu kuhusu usalama wa matumizi ya huduma za mawasiliano.
Kairuki alisema mamlaka zinazohusika zinaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya utapeli na uhalifu wa mtandao.
4G na 5G zaendelea kuenea
Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa huduma za 3G zimefikia asilimia 94.3 ya watu, huku 4G ikiwa imefikia asilimia 77.6 na 5G asilimia 34.
Kairuki alisema kiwango hicho kinaonesha kuwa changamoto kubwa kwa sasa siyo tu kujenga miundombinu ya mawasiliano, bali kuhakikisha wananchi wana vifaa vinavyowawezesha kutumia mitandao yenye kasi zaidi.
Alisema Serikali, kupitia Wizara ya Mawasiliano na taasisi zake kwa kushirikiana na sekta binafsi, inaendelea kushughulikia changamoto hizo kwa kuongeza upatikanaji wa huduma, vifaa na ujuzi wa kidijitali.
Minara yaongeza huduma vijijini
Alisema mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano unaendelea kuchangia upatikanaji wa huduma katika maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma za uhakika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi wa minara 1,798 uliozinduliwa na Serikali umewezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa takribani wananchi milioni 8.5 katika vijiji 1,400 kwenye mikoa 26 Tanzania Bara.
Kairuki alisema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kutambuliwa kimataifa kutokana na jitihada za kupanua huduma za mawasiliano katika maeneo ya pembezoni.
Huduma za utangazaji nazo zakua
Kwa upande wa utangazaji, idadi ya visimbuzi vilivyolipiwa iliongezeka kutoka milioni 2.29 Machi 2026 hadi milioni 2.26 Juni mwaka huo, huku mahitaji ya huduma za televisheni yakihusishwa pia na hamu ya wananchi kufuatilia mashindano makubwa ya michezo.
Aidha, huduma za redio za FM zimefikia asilimia 85 ya watu na asilimia 62 ya eneo la kijiografia la Tanzania.
Posta yakabiliwa na mabadiliko ya kidijitali
Katika huduma za posta na usafirishaji wa vifurushi, taarifa imeonesha mabadiliko ya matumizi yanayoendana na ukuaji wa teknolojia ya kidijitali.
Bidhaa za posta zilizotumwa kwenda nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 40.8, kutoka 32,565 Machi 2026 hadi 45,850 Juni mwaka huo.
Kwa upande mwingine, huduma za posta ndani ya nchi zimeendelea kukabiliwa na ushindani kutoka kwa mawasiliano ya kidijitali, ikiwemo barua pepe na majukwaa mengine ya mtandao.
Kairuki alisema mabadiliko hayo yanaonesha namna teknolojia inavyoendelea kubadilisha mahitaji na matumizi ya huduma za mawasiliano nchini.
Sekta ya mawasiliano yatajwa kuwa kichocheo cha uchumi
Waziri alisema Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni za mawasiliano, waendelezaji wa minara na wadau wengine kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua.
Aliwashukuru wadau wa sekta hiyo kwa mchango wao katika upanuzi wa huduma za mawasiliano nchini, akisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kutumia ipasavyo miundombinu hiyo ili kuongeza mchango wa sekta ya mawasiliano katika uchumi wa kidijitali na maendeleo ya kijamii.




