NCHIMBI AMTAKA BALOZI MKEREMY KUTANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI TANZANIA MALAYSIA
.DODOMA: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemtaka Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, kutumia nafasi hiyo kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Malaysia, hususan katika biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.
Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mkeremy mkoani Dodoma jana, Agosti 20, 2026, ambapo alisisitiza umuhimu wa kutumia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Malaysia kuongeza fursa za kiuchumi kwa Taifa.
Makamu wa Rais amempongeza Meja Jenerali Mkeremy kwa imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuwa mwakilishi wa Tanzania nchini Malaysia.
Amesema Malaysia ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa na ambayo Tanzania ina uhusiano wa kimkakati katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara na ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchimbi, Balozi Mkeremy anatakiwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuendeleza zaidi urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia, huku akihakikisha fursa za uwekezaji zinaongezeka na wawekezaji wengi zaidi kutoka Malaysia wanavutiwa kuwekeza nchini.
Aidha, amemtaka kuhamasisha Watanzania wanaoishi Malaysia, maarufu kama Diaspora, kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania.
Dkt. Nchimbi pia amemsisitiza Balozi huyo mteule kufahamu kwa kina Dira ya Taifa 2050 pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030, ili kuweza kutambua na kutekeleza ipasavyo vipaumbele vya Tanzania katika masuala ya uhusiano wa kimataifa.
Amesema uelewa huo utamsaidia Balozi Mkeremy kuelekeza nguvu katika maeneo yanayohitaji msisitizo wa kipekee na kuhakikisha diplomasia ya Tanzania inatumika ipasavyo katika kukuza maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, akieleza kuwa uteuzi huo ni dhamana kubwa kwake katika kulitumikia Taifa.
Pia amemshukuru Makamu wa Rais kwa nasaha alizompa na kuahidi kuzitumia katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akilenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia.






