PROF. SAID MOHAMED AANZA URAIS WA AEAA KWA AJENDA YA ELIMU JUMUISHI NA UBUNIFU
ARUSHA – Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohamed, amekubali rasmi kuwa Rais wa Jumuiya ya Tathmini za Kielimu Afrika (AEAA) kwa kipindi cha mwaka 2026–2027, akiahidi kuimarisha ushirikiano, uwazi na uwajibikaji katika uongozi wake.
Prof. Mohamed ametoa kauli hiyo jijini Arusha, wakati wa kufungwa kwa Mkutano wa 42 wa Mwaka wa AEAA.
Amesema kipaumbele chake ni kuilinda na kuiendeleza AEAA ili iendelee kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kutatua changamoto zinazokabili tathmini za kielimu barani Afrika..
Amesisitiza kuwa uongozi wake utazingatia ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja, akieleza kuwa mafanikio ya jumuiya yanategemea ushirikiano thabiti miongoni mwa wanachama.
Prof. Mohamed pia amesema mifumo ya elimu barani Afrika inapaswa kuendelea kubadilika ili kuendana na maendeleo ya Akili Unde (AI), elimu ya ujuzi, Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), pamoja na mahitaji ya sekta ya viwanda.
Amesema vijana ni rasilimali kubwa ya Afrika, hivyo elimu bora na yenye usawa ni msingi muhimu wa kujenga mustakabali wa bara hilo.
Aidha, ameahidi kuhakikisha uongozi wa AEAA unazingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji, ikiwemo kukabidhi madaraka kwa wakati, akieleza kuwa anatarajia kukamilisha mchakato huo Agosti 2027.








