Breaking News

RAIS SAMIA: JNHPP KUONDOA USUMBUFU KUKATIKA UMEME

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Kituo cha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) kitaongeza uwezo wa uzalishaji umeme na kuondoa usumbufu wa kukatika mara kwa mara kwa umeme.

Mkuu huyo wa nchi, ameyasema hayo leo, Agosti 22, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa JNHPP wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme na umegharimu Sh7.4 trilioni zote zimetolewa na Serikali.

Rais Samia, amesema uwezo huo wa uzalishaji umeongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, hatua itakayosaidia kuondoa usumbufu uliokuwa ukijitokeza katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema umeme wa uhakika utaimarisha uzalishaji viwandani, utoaji wa huduma hospitalini na matumizi ya wananchi majumbani, huku ukiwezesha shughuli mbalimbali kufanyika bila vikwazo vya umeme.

Amesema megawati zinazozalishwa na kituo hicho zimeongeza uwezo wa nchi kuzalisha umeme na kuwa na akiba ya kutosha, jambo litakalovutia uwekezaji, biashara, uzalishaji na ajira.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa ili umeme uwafikie wananchi wengi zaidi, akitaja kukamilika kwa njia ya Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa kituo cha Zuzu.