Breaking News

WAZIRI NDEJEMBI: JNHPP KUIFANYA TANZANIA KUWA KIUNGANISHI SOKO LA NISHATI KIKANDA

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kukamilika na kuzinduliwa rasmi kwa Mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) kumeongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme na kuiweka nchi katika nafasi muhimu ya kuunganisha soko la nishati la kikanda.

Amesema kukamilika kwa mradi huo ni matokeo ya juhudi mahususi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha JNHPP inakamilika na kuanza kutoa mchango wake katika kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

“Uzinduzi wa Mradi wa Julius Nyerere ni matokeo ya juhudi zako mahususi kuhakikisha mradi huu unakamilika,” amesema Ndejembi.

Amesema JNHPP ina mitambo tisa, ambapo kila mmoja una uwezo wa kuzalisha megawati 235, na kufanya jumla ya uwezo wa uzalishaji kufikia megawati 2,115. Uwezo huo utaisaidia Tanzania kukidhi mahitaji ya umeme kwa shughuli za kiuchumi na uwekezaji.

“Hii inatufanya tuwe daraja muhimu la kuunganisha soko kubwa la nishati barani Afrika kwani nchi yetu ni mwanachama wa Eastern Africa Power Pool na Southern Africa Power Pool, ambapo Tanzania inaunganisha mtandao wa umeme kikanda,” amesema Ndejembi.