SHEIKH JALALA: UMOJA, MAADILI NA AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO YA TANZANIA
DAR ES SALAAM: Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Shia Ithna'Asheriyyah Tanzania (TIC), Sheikh Hemmed Jalala, amewataka Watanzania kuenzi mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.W.) kwa kudumisha amani, umoja, maadili na mshikamano wa kitaifa.
Sheikh Jalala ameyasema hayo wakati wa matembezi ya kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad (S.A.W.W.), akieleza kuwa kipindi hicho kinapaswa kuwa fursa ya kutafakari mafundisho ya Mtume na kuyatumia kujenga jamii yenye huruma, upendo na mshikamano.
Amesema moja ya mafundisho muhimu ya Mtume ni huruma na upendo, akisisitiza kuwa jamii ya sasa inahitaji kurejesha misingi hiyo kutokana na changamoto za kupungua kwa mshikamano na maelewano miongoni mwa watu.
Kwa mujibu wa Sheikh Jalala, jambo jingine muhimu ni maadili na tabia njema, akieleza kuwa maadili huanzia ndani ya familia kabla ya kuenea katika jamii na kufika katika ngazi za mamlaka.
“Dunia imepoteza maadili, Waafrika wamepoteza mila zao, wamepoteza desturi zao na taratibu zao,” amesema Sheikh Jalala, akisisitiza umuhimu wa kurejesha maadili katika jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa Waislamu, akiwataka Mashia, Masunni na wafuasi wa madhehebu mengine kukaa pamoja na kushirikiana kama watu wa familia moja.
Amesema umoja huo unapaswa kwenda sambamba na umoja wa kitaifa, akisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kushirikiana bila kujali tofauti za dini na misimamo yao.
“Umoja wetu wa kitaifa, umoja wetu kama Watanzania ndiyo sababu kubwa itakayoleta maendeleo,” amesema.
Sheikh Jalala pia ametoa wito wa kulinda amani, akisema malalamiko, madai na harakati mbalimbali katika jamii yanapaswa kufanyika kwa njia za amani.
Amesema amani, utulivu na mshikamano ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa.
Katika hatua nyingine, Sheikh Jalala amewataka vijana kutumia vyema nafasi waliyonayo katika kujenga taifa, akiwataka kuwa watafiti, kuchambua taarifa wanazozipokea na kuepuka kuchukua mambo juu juu.
Amesema vijana wanapaswa kuzingatia maadili na kutumia nguvu zao katika maendeleo badala ya kuwa chanzo cha kuvuruga nchi.
“Vijana ndio chachu ya maendeleo ya nchi, kwa hiyo wasiwe sababu ya kuvuruga nchi yao, wawe sababu ya kuitengeneza nchi yao,” amesema.
Kwa upande wake, Sheikh Rehani Yassin amesema vijana wanapaswa kutumia fursa ya ujana wao kwa kujifunza, kutafuta elimu na kuchambua taarifa kwa umakini kabla ya kufanya maamuzi.
Akitaja miongoni mwa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.W.), Sheikh Yassin amesema vijana wanapaswa kunufaika na ujana wao kabla ya kufikia uzee, akiwataka kutotumia ujana wao kwa mhemko au kufanya maamuzi ya haraka.
Amesema katika kipindi ambacho taarifa zinaenea kwa kasi, vijana wanapaswa kuwa na uwezo wa kutafiti na kuthibitisha taarifa kabla ya kuziamini au kuzisambaza.
Sheikh Yassin amesisitiza kuwa upotoshaji wa taarifa unaweza kutumiwa kuwachochea au kuwapotosha vijana, hivyo akawataka kuwa makini na taarifa wanazokutana nazo katika jamii na kwenye mitandao ya kijamii.
Amesema vijana ni nguvu kazi ya taifa na kwamba iwapo wataelimishwa na kuelekezwa vizuri, wanaweza kuwa sehemu muhimu ya kujenga Tanzania yenye amani, umoja na maendeleo.













