TANZANIA YAKANA TUHUMA ZA KUINGILIA UCHAGUZI ZAMBIA
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekanusha tuhuma zilizotolewa na mgombea Urais wa Chama cha NRPUP nchini Zambia, Brian Mundubile, kwamba Tanzania imetuma watu nchini humo kwa lengo la kuingilia na kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa Zambia uliofanyika Agosti 13, 2026.
Msigwa amesema Serikali ya Tanzania imezisikia tuhuma hizo na imezichukulia kwa uzito, huku ikiwahakikishia Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania haijamtuma mtu yeyote nchini Zambia kwa lengo la kuingilia au kuvuruga uchaguzi huo.
Amesema Tanzania haina utamaduni wa kuingilia uchaguzi wa nchi nyingine na kwamba kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, Serikali imeiandikia Serikali ya Zambia kutaka maelezo ya kina kuhusu sababu za mgombea huyo kutoa tuhuma hizo.
Msigwa amesema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ina uwakilishi wa waangalizi wa uchaguzi nchini Zambia.
Amefafanua kuwa waangalizi hao wanafanya kazi kwa kuzingatia miongozo ya waangalizi wa uchaguzi ya SADC, sambamba na waangalizi wengine waliopo nchini Zambia, na kwamba uwepo wao ni kwa ajili ya uangalizi wa uchaguzi, siyo kuingilia au kuvuruga mchakato huo kama ilivyodaiwa na Mundubile.




