Breaking News

TBA YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KATIKA MAENEO 308 KUENDELEZA MIRADI YA UJENZI

DODOMA: Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umewaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa za maeneo 308 yaliyotangazwa kwa ajili ya uwekezaji, yakihusisha ujenzi wa majengo ya makazi, biashara, viwanda na miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumza kuhusu fursa hizo, Mkurugenzi wa Huduma Msaidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, amesema marekebisho ya sheria ya Wakala yaliyofanyika Agosti 2023 yamewezesha taasisi hiyo kufanya kazi kwa karibu zaidi na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uwekezaji.

Amesema TBA, ambayo iko chini ya Wizara ya Ujenzi, ina ofisi katika mikoa yote 26 na tayari imefanya upembuzi yakinifu katika maeneo zaidi ya 147 ambayo yameiva kwa ajili ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa Bi. Lumuli, fursa zilizopo zinahusisha ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na majengo ya kibiashara, ikiwemo shopping malls na miradi mingine inayoweza kuongeza shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Amesema TBA pia imeweka mkazo katika kuunga mkono sekta ya kilimo na mifugo kwa kutumia utaalamu wake wa ujenzi kubuni na kujenga miundombinu inayoweza kuongeza thamani ya mazao na kupunguza upotevu baada ya mavuno.

Ameeleza kuwa miongoni mwa fursa hizo ni ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao, ambayo yatawawezesha wakulima kuhifadhi bidhaa zao katika mazingira bora kabla ya kuzipeleka sokoni.

“Tunafahamu mazao yakihifadhiwa vizuri bei yake sokoni inaweza kuwa nzuri na yenye tija kwa mkulima,” amesema.

Aidha, amesema TBA ina uwezo wa kujenga miundombinu ya kuhifadhi mazao yanayohitaji mazingira ya ubaridi, ikiwemo samaki, nyama, mboga mboga na matunda, ili kuhakikisha yanabaki katika ubora unaohitajika hadi yanapofikishwa sokoni.

Amesema miundombinu hiyo itasaidia wakulima na wafugaji kupata thamani zaidi ya bidhaa zao na kupunguza hasara zinazoweza kutokana na uharibikaji wa mazao.

Bi. Lumuli amesema TBA pia iko tayari kushirikiana na wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao katika maeneo hayo, hatua ambayo itaongeza thamani ya bidhaa za wakulima kabla ya kuuzwa sokoni.

Ametolea mfano kuwa badala ya mkulima kuuza mahindi kama yalivyo, anaweza kuyauza baada ya kuchakatwa kuwa unga, huku mpunga ukiweza kuchakatwa na kuuzwa kama mchele.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao, kuongeza kipato kwa wakulima na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Tunawakaribisha wawekezaji ambao wanaweza kufanya viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali katika maeneo yetu. TBA iko tayari kushirikiana nao kwa aina mbalimbali za uwekezaji,” amesema.

Ameongeza kuwa fursa hizo hazilengi wakulima na wafugaji pekee, bali zinawahusu Watanzania na wawekezaji wote wanaotaka kutumia maeneo ya TBA kuanzisha miradi yenye tija kwa uchumi.