LONDO: TANZANIA ITUMIE TAARIFA ZA MASOKO KUONGEZA USHINDANI WA BUDHAA DUNIANI
DODOMA: Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Londo, amesema Tanzania inapaswa kutumia taarifa sahihi za masoko kama nyenzo muhimu ya kuongeza ushindani wa bidhaa zake katika masoko ya kikanda na kimataifa, badala ya kuzichukulia kama taarifa za kawaida.
Amesema matumizi sahihi ya taarifa hizo yatasaidia kuharakisha mageuzi ya uchumi na kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo nchini.
Londo aliyasema hayo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, katika hafla iliyoandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwenye Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Alisema dunia ya biashara inabadilika kwa kasi kutokana na mabadiliko ya mahitaji ya walaji, viwango vya ubora, matumizi ya teknolojia za kidijitali pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo Tanzania haina budi kwenda sambamba na mwelekeo huo.
Kwa mujibu wa Londo, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2023 pamoja na programu mbalimbali za maendeleo ya kilimo unahitaji uzalishaji unaoongozwa na mahitaji halisi ya soko, badala ya kuzalisha kwanza na kutafuta wanunuzi baadaye.
Alisisitiza umuhimu wa taasisi zinazohusika na sekta za kilimo, biashara na uwekezaji, mamlaka za udhibiti, taasisi za fedha, serikali za mitaa pamoja na sekta binafsi kushirikiana kuhakikisha taarifa za masoko zinawafikia wadau kwa wakati.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kuhusu uzalishaji, uongezaji thamani na biashara ya mazao.
Londo aliongeza kuwa mafanikio ya Tanzania hayapaswi kupimwa kwa ongezeko la mauzo ya bidhaa nje ya nchi pekee, bali pia kwa kuongezeka kwa ajira, mapato ya wananchi na ukuaji wa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao.
Alisema nafasi ya kijiografia ya Tanzania, inayopakana na nchi nane, inatoa fursa kubwa kwa nchi kuwa kitovu cha biashara ya mazao ya kilimo, endapo kutakuwa na uratibu mzuri wa uzalishaji, uongezaji thamani na biashara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa utaratibu wa Shoroba Tanzania (AGCOT), Geoffrey Kirenga, amesema matumizi ya sayansi na teknolojia yanaweza kusaidia Tanzania kufikia masoko mbalimbali duniani kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko hayo.




