TMA YATOA TAHADHARI YA EL NINO, SEKTA ZATAKIWA KUJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Bakari, amezitaka sekta zote nchini kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa katika kufanya maandalizi ya kisekta ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na El Niño.
Jaji Mshibe amesema hayo mkoani DODOMA wakati akifungua Mkutano wa 25 wa kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli, Oktoba hadi Disemba 2026.
“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa mvua za Vuli, Oktoba hadi Disemba 2026, ni muhimu kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu na kuelewa taarifa hizo ili kuanza maandalizi ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na athari za hali ya hewa zinazotarajiwa kujitokeza katika sekta yake, kwa kutambua kuwa upo uwezekano mkubwa kwa El Niño kuendelea kuimarika kuelekea mwishoni mwa mwaka 2026,” alisisitiza Jaji Mshibe.
Jaji mshibe amesema Tanzania, inaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayodhihirishwa kupitia ongezeko la joto, ukame, upepo mkali, vimbunga na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko, hivyo amewataka wadau wasiishie katika kupokea taarifa za utabiri wa hali ya hewa, bali wazitumie katika kufanya maamuzi yanayozingatia mazingira ya sekta na maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema TMA imeendelea kuboresha utoaji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwemo kuandaa utabiri mahususi kwa maeneo madogo kwa wilaya 86 zilizopo katika mikoa inayopata mvua za Vuli, hatua inayolenga kuhakikisha kila wilaya na sekta husika zinaweza kutumia taarifa za hali ya hewa katika kufanya maamuzi na kupanga shughuli zao
Mkutano huo umebeba kaulimbiu: “Kupunguza Pengo la Uelewa wa Tahadhari za Hali ya Hewa kwa Pamoja.” na kuhusisha utoaji wa mrejesho kutoka kwa wadau kuhusu utabiri wa msimu wa mvua za Masika uliokuwa na usahihi wa asilimia 94.1.




