Breaking News

TTCL KUANZA KUSAMBAZA FIBER MLANGONI KWA WANANCHI NCHI NZIMA

DAR ES SALAAM – Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeanza kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa “Fiber Mlangoni Kwako” (FTTH), unaolenga kusambaza huduma ya intaneti ya kasi kwa wananchi, taasisi na maeneo ya biashara katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza katika uzinduzi wa awamu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Julai 2026 na unahusisha ujenzi wa maunganisho 400,000 (home pass), hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya maunganisho ya TTCL hadi takribani 750,000 ifikapo Juni 2027.

Marwa amesema mpango wa shirika ni kufikisha maunganisho hayo hadi milioni moja ifikapo Juni 2028, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka 10 wa TTCL unaoanzia mwaka 2025/26 hadi 2034/35.

Amesema mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi, yenye ubora na gharama nafuu, huku ukichangia katika utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Marwa, TTCL imeamua kutumia teknolojia ya kisasa ya GPON, ambayo ina uwezo wa kuunganisha wateja wengi kwa wakati mmoja, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma ikilinganishwa na teknolojia ya awali ya Point-to-Point.

Amesema awamu ya kwanza ya mradi huo ilitekelezwa katika maeneo yaliyochaguliwa kimkakati katika Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Mbeya, Mwanza na Unguja Zanzibar, ambapo takribani maunganisho 38,000 yalijengwa kwa kutumia teknolojia ya GPON.

“Awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu huduma za intaneti zitafika katika mikoa yote nchini kwa maana ya Tanzania Bara pamoja na Visiwani,” amesema Marwa.

Ameongeza kuwa upanuzi huo wa mtandao wa fiber optic utaiwezesha TTCL kuwafikishia wananchi na taasisi huduma za mawasiliano na intaneti ya kasi, huku ukisaidia kuongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali nchini.

Marwa amesema mradi huo pia ni sehemu ya mkakati wa TTCL wa kuongeza idadi ya wateja, mapato na kuboresha huduma, sambamba na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa shirika.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unafanywa kwa kushirikiana na wakandarasi Huawei, ZTE na FiberHome, ambao tayari wameanza maandalizi ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi na kuimarisha ushiriki wa wananchi, taasisi za umma na binafsi katika uchumi wa kidijitali.