WAZIRI KAIRUKI AIAGIZA TTCL KUFIKIA NYUMBA MILIONI MOJA HUDUMA YA FIBER MLANGONI IFIKAPO 2028
DAR ES SALAAM – Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, ameiagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya uunganishaji wa huduma ya intaneti ya mkongo wa nyuzi majumbani (FTTH) ili kufikisha huduma hiyo katika nyumba milioni moja ifikapo Juni 2028.
Kairuki ametoa agizo hilo leo, Agosti 21, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi awamu ya pili ya mradi wa “Fiber Mlangoni Kwako”, unaotekelezwa na TTCL kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi, ubora na uhakika kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema awamu hiyo inalenga kuongeza wigo wa huduma hadi kufikia home passes 500,000, kabla ya kufikia nyumba milioni moja ifikapo Juni 2028, akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayatapaswi kupimwa kwa idadi ya nyumba ambazo fiber imepita pekee, bali pia idadi ya wateja wanaounganishwa na ubora wa huduma.
“Hatupaswi kuridhika na fiber kupita mbele ya nyumba ikiwa kaya haiwezi kujiunga. Hatupaswi kuridhika na usajili ikiwa huduma haitimizi ahadi ya kasi na uhakika,” amesema.
Kwa mujibu wa Kairuki, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026 zinaonyesha kuwa usajili wa intaneti nchini ulifikia milioni 62.7, huku matumizi ya data yakifikia petabytes 1,041.
Hata hivyo, amesema watumiaji wa huduma ya fiber majumbani walikuwa 178,904 pekee, hali inayodhihirisha pengo lililopo kati ya mahitaji ya intaneti na upatikanaji wa huduma hiyo kwa kaya.
Ameitaka TTCL kupanua huduma katika maeneo yanayokua kwa kasi, vituo vya biashara, masoko, maeneo ya viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, amelitaka shirika hilo kurahisisha taratibu za usajili, kupunguza muda wa kuunganisha huduma na kushirikiana na serikali za mitaa, waendelezaji wa makazi, wamiliki wa majengo na jumuiya za wafanyabiashara ili kuongeza idadi ya watumiaji.
Kairuki pia ameitaka TTCL kubuni vifurushi vinavyoweza kumudu kaya na makundi mbalimbali, wakiwemo wanafunzi, vijana, wafanyakazi, wavuvi, wachimbaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na taasisi, akisisitiza kuwa gharama za kuunganisha huduma, vifaa na vifurushi hazipaswi kuwa kikwazo.
Katika kuboresha huduma kwa wateja, ameitaka TTCL kuimarisha ufuatiliaji wa mtandao, matengenezo ya kinga na urejeshaji wa huduma kwa haraka, pamoja na kuweka mifumo rahisi ya kupokea na kufuatilia malalamiko.
Amesema mteja hapaswi kulazimika kufuatilia mwenyewe tatizo aliloripoti, bali TTCL inapaswa kumjulisha hatua zilizofikiwa na kuhakikisha changamoto yake inatatuliwa kwa wakati.
Waziri huyo pia ameitaka TTCL kusimamia kwa karibu wakandarasi na wazabuni wanaotekeleza miradi hiyo ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia mikataba.
Amesema Serikali inalenga kuona TTCL ikiwa na zaidi ya wateja milioni mbili hadi milioni tatu wanaotumia huduma za fiber majumbani ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Abubakar Asenga, ameishauri Serikali kuongeza uwekezaji na bajeti kwa TTCL ili kuwezesha upanuzi zaidi wa huduma za intaneti kupitia mradi huo.
Asenga amesema Bunge kupitia Kamati hiyo limekuwa likisisitiza kwa miaka kadhaa umuhimu wa kuimarisha TTCL ili iweze kuwa chombo muhimu katika kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kuongeza mapato ya Taifa.
Amesema hadi mwaka wa fedha 2024/25, TTCL ilikusanya takribani Sh bilioni 100 kupitia kuunganisha wateja wapatao 280,000.
Kwa mujibu wa Asenga, mpango ni kufikisha mapato ya takribani Sh bilioni 400 ifikapo mwaka 2029 baada ya kuunganisha wateja milioni moja, huku idadi ya wateja milioni mbili ikiweza kulifikisha shirika kwenye mapato yanayokaribia Sh trilioni moja ifikapo mwaka 2030.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema awamu ya pili ya mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka 10 wa shirika, unaoanzia mwaka 2025/26 hadi 2034/35.
Marwa amesema mpango huo unalenga kuboresha huduma, kuongeza idadi ya wateja na mapato, kuimarisha uendeshaji wa kielektroniki, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Amesema TTCL imeanza kutumia teknolojia ya GPON inayowezesha kutoa intaneti yenye kasi kubwa, kuunganisha wateja wengi kwa wakati mmoja, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma ikilinganishwa na teknolojia ya Point-to-Point.
Amesema awamu ya kwanza ya mradi ilitekelezwa katika maeneo ya kimkakati ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Mbeya, Mwanza na Unguja Zanzibar, ambapo takribani home pass 38,000 zilijengwa, huku mtandao uliokuwa umejengwa awali kwa teknolojia ya Point-to-Point ukifikisha maunganisho takribani 33,000.
Kwa mujibu wa Marwa, utekelezaji wa awamu ya pili ulianza Julai 2026 na jumla ya home pass 400,000 zinatarajiwa kujengwa.
“Mpango huu utapelekea takribani maunganisho 750,000 kuwa yamejengwa kufikia Juni 2027, na mpango wa Shirika ni kufikia maunganisho takribani milioni moja ifikapo Juni 2028,” amesema.
Amesema utekelezaji wa mradi huo utaongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali nchini.














