UDOM YAHIMIZA WANAFUNZI KUKAMILISHA UDAHILI 2026/2027, YAANZISHA PROGRAM TANO MPYA
DODOMA: Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewahimiza waombaji wa elimu ya juu kutumia siku chache zilizobaki kukamilisha maombi ya udahili wa mwaka wa masomo 2026/2027, huku kikitangaza kuanza kwa programu tano mpya za shahada ya kwanza.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Udahili wa chuo cha UDOM,, Dostea chalamila, alisema chuo kinaendelea kutoa huduma za udahili wa papo kwa papo katika banda lake ili kuwawezesha waombaji kukamilisha maombi yao kwa urahisi.
Alisema dirisha la kwanza la udahili linakaribia kufungwa, hivyo wanafunzi wote wenye sifa wanapaswa kutumia muda uliosalia kuwasilisha maombi yao na kujiunga na UDOM.
Lamila alisema kwa mwaka wa masomo 2026/2027, UDOM imeanzisha programu tano mpya ambazo ni Bachelor of Medical Laboratory Science, Bachelor of Crop Production and Technology, Bachelor of Biomedical Engineering, Bachelor of Counselling Psychology, na Bachelor of Business with Education.
Alifafanua kuwa programu hizo zimeongezwa ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza fursa za masomo kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari na wale wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu.
Aidha, aliwataka waombaji kuhakikisha wanasoma kwa makini vigezo vya udahili vilivyobainishwa katika Guidebook ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) pamoja na mwongozo wa UDOM kabla ya kuchagua programu wanazotaka kuomba.
Lamila alisisitiza kuwa UDOM inaendelea kupokea waombaji katika banda lake lililopo Nanenane, ambapo huduma za ushauri na udahili wa papo kwa papo zinapatikana kwa wote wanaotaka kujiunga na chuo hicho.
"Karibuni Chuo Kikuu cha Dodoma. Tunawahimiza waombaji wote wenye sifa kutumia fursa hii na kukamilisha udahili wao ndani ya muda uliobaki," alisema.




