Breaking News

CEMEX VENTURES YAJIVUNIA UZALISHAJI WA MAFUTA BORA, YAHAMASISHA MATUMIZI YA MAFUTA YA ALIZETI YA NDANI

DODOMA: Kampuni ya CEMEX Ventures Limited imesema imejipanga kuongeza uzalishaji wa mafuta halisi ya alizeti yaliyosafishwa kwa kiwango cha juu (Double Refined) ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa, hatua itakayosaidia kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wa Tanzania.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Diana Morandi, alisema kampuni hiyo yenye makao yake Kizota, Dodoma, huzalisha mafuta ya alizeti yanayojulikana kwa jina la Golden Harvest, huku maonesho hayo yakitumika kuwaonesha wananchi mchakato mzima wa uchakataji na uzalishaji wa mafuta hayo.

Alisema kwa sasa kampuni inasambaza bidhaa zake katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na Tabora, huku ikilenga kupanua zaidi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Morandi alisema ushirikiano kati ya kampuni hiyo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kuwafikia wakulima moja kwa moja na kupata malighafi zenye ubora unaokidhi viwango vya uzalishaji.

Alieleza kuwa kampuni hupima ubora wa mbegu za alizeti kwa kuangalia kiwango cha unyevu (moisture) pamoja na kiwango cha mafuta kilichomo ndani ya mbegu kabla ya kuzitumia katika uzalishaji, jambo linalohakikisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Aidha, alisema kupitia ushirikiano huo, wakulima wamekuwa wakipata pembejeo bora zinazowawezesha kuongeza uzalishaji wa alizeti, huku kampuni ikihakikishiwa upatikanaji wa malighafi za kutosha kwa uzalishaji endelevu mwaka mzima.

Morandi alibainisha kuwa TADB pia imekuwa ikiisaidia kampuni kwa huduma za kifedha pamoja na kuwezesha upatikanaji wa maghala ya kuhifadhi malighafi, hatua inayowezesha uzalishaji wa mafuta kuendelea bila kukatizwa katika kipindi chote cha mwaka.

Alisema kampuni inalenga kupanua wigo wa masoko ya kimataifa kutokana na ubora wa mafuta yake yaliyosafishwa, huku akisisitiza kuwa matumizi ya mbegu zinazozalishwa na wakulima wa Tanzania yataongeza thamani ya mazao ya ndani, kukuza uchumi na kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.