GST YATAKA WACHIMBAJI KUTUMIA TAARIFA ZA KISAYANSI KATIKA UCHIMBAJI
GEITA - Taasisi ya Jeolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepanga kuongeza eneo la utafiti wa madini kwa kutumia ndege (High-Resolution Airborne Geophysical Survey) kutoka asilimia 16 hadi asilimia 50 ya eneo la Tanzania katika mwaka huu wa fedha.
Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita mwaka 2026, Mkuu wa Ofisi ya GST-Geita, Johnson Muhozi, amesema utafiti huo utasaidia kuongeza taarifa kuhusu uwepo wa rasilimali madini nchini na kuwawezesha wachimbaji kufanya shughuli zao kwa tija zaidi.
Muhozi amesema taarifa zitakazopatikana kupitia utafiti huo zitasaidia kuwaongoza wachimbaji wadogo katika maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa rasilimali madini, huku pia zikisaidia kuongeza taarifa za rasilimali zilizopo nchini na hivyo kuchangia kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini.
Amesema GST pia itaendelea kufanya tafiti za madini kwa kutumia sehemu ya asilimia 10 ya mapato yatokanayo na makusanyo katika sekta ya madini kupitia Tume ya Madini, fedha ambazo zinalenga kusaidia taasisi hiyo kufanya utafiti na kuongeza taarifa za rasilimali madini nchini.
Mbali na utafiti, Muhozi amesema GST inatoa huduma mbalimbali ikiwemo utafiti wa madini, ushauri wa kitaalamu katika hatua za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini, pamoja na ushauri kuhusu uchukuaji sahihi wa sampuli kwa ajili ya vipimo vya maabara.
Amesema maabara za GST hufanya upimaji wa sampuli mbalimbali ikiwemo miamba, udongo, vimiminika (solution), kaboni na sampuli nyingine kwa lengo la kubaini aina na kiwango cha madini yaliyopo.
Katika maonesho hayo, GST pia imeendelea kutoa na kuuza vyungu maalumu vya maabara vinavyofahamika kama crucible, vinavyotumika katika upimaji wa sampuli za dhahabu na madini mengine yanayoambatana na dhahabu.
Muhozi amesema upatikanaji wa crucible hizo nchini kupitia GST unatoa fursa kwa wadau wa sekta ya madini kupata bidhaa hiyo ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje.
Aidha, amewaalika wachimbaji wadogo, wachimbaji wa kati na wakubwa pamoja na wananchi kwa ujumla kutembelea banda la GST katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema ofisi za GST zinapatikana Geita, mtaa wa Maganya Malembo, jirani na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi (RMO), pamoja na makao makuu yaliyopo Dodoma, ambapo wananchi na wadau wanaweza kupata huduma mbalimbali za taasisi hiyo.
Hatua hizo zinaendana na utekelezaji wa dira ya sekta ya madini inayolenga kuimarisha upatikanaji wa taarifa za rasilimali madini nchini kwa kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri.




