Breaking News

MBOGWE YATANGAZA FURSA ZA KIUCHUMI KUPITIA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

GEITA: Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imeshiriki katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, ikitumia fursa hiyo kutangaza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali wa wilaya hiyo pamoja na kutoa elimu kuhusu ufugaji nyuki, ufugaji wa kuku na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Renatus Kamara, amesema Halmashauri hiyo imefika katika maonesho hayo ikiwa na bidhaa mbalimbali kwa lengo la kuwafahamisha wananchi kuhusu fursa za kiuchumi zinazopatikana Mbogwe, pamoja na kuwaunganisha wazalishaji na masoko.

Kamara amesema miongoni mwa bidhaa zinazopatikana katika banda la Halmashauri hiyo ni asali ya masega, asali iliyochakatwa na kufungashwa, mchele pamoja na kuku wanaofugwa na wajasiriamali wa Mbogwe.

Amesema asali ya masega ni miongoni mwa bidhaa zinazopatikana moja kwa moja kutoka kwenye mizinga bila kupitia mchakato mkubwa wa uchakataji, huku aina nyingine ya asali ikiwa imechakatwa na kufungashwa tayari kwa matumizi.

«“Tumekuja hapa tukiwa na bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuwaonyesha watu, kuwaeleza ujuzi na kuuza bidhaa zinazopatikana katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Mbogwe,” amesema Kamara.»

Aidha, amesema maonesho hayo yanatumika pia kutoa elimu kuhusu ufugaji wa nyuki na uhifadhi wa mazingira, akiwataka wananchi kutembelea banda la Halmashauri ya Mbogwe ili kujifunza na kuona bidhaa zinazozalishwa katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, mjasiriamali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Joshua Mbala, amesema wamewasilisha bidhaa mbalimbali ikiwemo asali, kuku, mchele na karanga, huku wakitoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki na kuku.

Mbala amesema wananchi wanaotembelea banda hilo pia wanapata elimu kuhusu matumizi ya mashine za kukamulia asali, hatua inayolenga kuboresha uzalishaji na uchakataji wa asali.

Ameongeza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza mbinu bora za ufugaji na kupata bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Mbogwe.

Hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imewataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali kutembelea banda lake katika maonesho hayo, kujifunza kuhusu shughuli za uzalishaji na kupata bidhaa mbalimbali zinazozalishwa wilayani humo.

Maonesho hayo yanaendelea mkoani Geita, yakilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wajasiriamali na wananchi ili kubadilishana maarifa, teknolojia na fursa za kiuchumi.