Breaking News

RC TANGA: KUMBATIENI MIFUMO YA KIDIJITI KULINDA MAFAO

Tanga - Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amewataka wastaafu kulinda mafao yao dhidi ya matapeli, huku akiupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorudisha heshima na tabasamu kwa wastaafu.

Akifungua semina ya PSSSF kwa waajiri iliyofanyika jijini Tanga iliyowakutanisha Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala 120 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, Balozi Dkt. Batilda alieleza kuwa maboresho hayo yanaendana na maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora, za haraka na bila vikwazo.

"Niwapongeze sana PSSSF kwa hatua hii inaowezesha Mafao kulipwa kwa haraka," alisema.

Meneja wa PSSSF Kanda ya Kaskazini Mashariki, Bw. Kwame Temu, aliwahimiza waajiri kutoa taarifa za watumishi wapya ndani ya siku 30 ili wasajiliwe mapema na kuwahamasisha watumishi kutumia kikamilifu mifumo ya kielektroniki. Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Mkoa wa Tanga, Bi. Hanim Babika, alisisitiza waajiri kufanyia kazi changamoto ya kugongana kwa taarifa na kuhakikisha wafanyakazi wa mikataba kusajiliwa.

Akitoa ushuhuda, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta alisema elimu inayotolewa na PSSSF imebadili kabisa maisha ya wastaafu wa sasa, kwani wanatoka utumishi wakiwa wanajiamini na wenye uelewa mpana wa uwekezaji. 

"Sekretari wangu alipostaafu, alikuja ofisini kwangu mwenye furaha, ananieleza habari za fursa za uwekezaji tu baada ya kupata mafunzo ya PSSSF," alisema Katibu Tawala.

PSSSF inaendelea kuwasihi wanachama na wastaafu nchini kutumia mifumo rasmi ya kielektroniki ili kupata huduma kwa haraka, uwazi na usalama zaidi ambayo ni PSSSF Member Portal na PSSSF Kiganjani. Aidha, wanachama wanashauriwa kutumia namba ya simu ya bure kuwasiliana na Mfuko ambayo ni 080011005