Breaking News

SERIKALI YASISITIZA MATOKEO CHANYA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050

Serikali imeweka wazi msimamo wake thabiti wa kutaka kuona matokeo ya moja kwa moja ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 badala ya kujikita katika michakato isiyo na tija inayochelewesha maendeleo. 

Akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Wanamipango lililofanyika jijini Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisisitiza kuwa taasisi za umma zinalazimika kuonyesha matokeo yanayopimika badala ya kutegemea mlolongo mrefu wa kisheria na kiutawala ambao haukamiliki kwa wakati. 

Alionya dhidi ya utamaduni wa kujitetea kwa shughuli za kila siku huku kukiwa hakuna mafanikio halisi yanayoonekana, akibainisha kuwa wakati umefika wa watumishi na taasisi kupimwa kwa matokeo ya kazi zao badala ya idadi ya makaratasi na madokezo yanayozunguka kwenye mifumo ya ofisi.

Profesa Kitila alifafanua kuwa mafanikio ya Dira 2050 yalianzia katika ngazi za chini za utekelezaji, hususan katika mamlaka za serikali za mitaa ambazo zinatakiwa kubadilisha mitazamo yao na kuwa wawezeshaji wakuu wa sekta binafsi badala ya kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara na wakulima. 

Alisema ni jambo lisilokubalika kuona wakulima wakipambana peke yao wakati wa kilimo lakini wakikutana na vikwazo mbalimbali pindi wanapomaliza kuvuna mazao yao. 

Aidha, serikali imesisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu, hususan kupitia elimu inayojenga uwezo wa kiakili, afya ya mwili, na maadili mema, ni nguzo isiyoweza kukwepeka katika safari ya kufikia malengo ya Dira ya 2050.