SERA ZA UCHUMI ZA TANZANIA ZANG'ARA KIMATAIFA KWA BoT KUNYAKUA TUZO TANO
Tanzania imeweka historia kubwa katika uga wa kimataifa baada ya kuibuka na tuzo tano kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jambo linalothibitisha kukubalika na kuaminika kwa sera za kiuchumi na za huduma jumuishi za kifedha zinazotekelezwa nchini.
Tuzo hizo zilitolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) duniani, zikiwemo Tuzo ya Azimio la Maya inayotambua mafanikio ya nchi katika kuweka, kupima, na kutekeleza ahadi za kuendeleza huduma jumuishi za fedha.
Vyeti hivyo vya utambuzi vilipokelewa rasmi na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, wakati wa Jukwaa la Kimataifa la Sera za Huduma Jumuishi za Fedha la mwaka 2026 lililofanyika Port Moresby, Papua New Guinea.
Mafanikio haya yametokana na utekelezaji madhubuti wa mikakati mbalimbali, ikiwemo Mkakati wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2023 hadi 2028.
akwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha ujumuishi wa kifedha nchini kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2023, huku vipimo vya ndani vikiashiria kupanda hadi asilimia 80.
Sambamba na hilo, idadi ya watu wazima wasio na huduma za kifedha imepungua kwa kiasi kikubwa kutoka milioni 7.8 hadi milioni 6.4, huku upatikanaji wa huduma hizo ndani ya umbali wa kilometa tano ukiongezeka kutoka asilimia 86 hadi 89, na matumizi ya fedha za simu yakipanda hadi asilimia 72.
Mbali na mafanikio hayo ya jumla, BoT itatambuliwa kwa jinsi inavyotekeleza Mpango Kazi wa Denarau unaolenga kuendeleza huduma jumuishi za fedha kwa wanawake na kupunguza pengo la kijinsia.
Kupitia sera zinazojumuisha masuala ya jinsia na kupunguza vikwazo vya mikopo kwa wanawake, pengo la huduma za kifedha kati ya wanawake na wanaume limepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.2 mwaka 2022.
Aidha, tuzo mbili za kibinafsi zilitolewa kwa watumishi wa BoT, Dk. Khadija Kishimba na Nangi Massawe, kwa kutambuliwa katika uongozi wa kiufundi na sera za huduma jumuishi za kifedha, wakati Meneja wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Mutashobye Mushumbusi, akieleza kuwa benki hiyo imeweka mwongozo maalum wa kupunguza gharama za huduma za kifedha ili kuwapunguzia mzigo wananchi.




