SERIKALI YAPIGA HATUA KULINDA WATOTO MTANDAONI
Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni imefanikiwa kuwafikia watoto 1,811,212 na kuwapatia elimu muhimu ya kujikinga na hatari za kidijiti.
Kauli hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Maryprisca Mahundi, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Kombani, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni kutokana na wimbi kubwa la matumizi ya teknolojia.
Katika majibu yake, Naibu Waziri alisisitiza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha watoto wananufaika na fursa za kidijiti huku wakiwa salama dhidi ya unyanyasaji, unyonyaji na madhara yote yanayotokana na matumizi yasiyo salama ya mtandao.
Sehemu kubwa ya mafanikio hayo imetokana na utekelezaji wa kampeni hiyo iliyofika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ikiwa na lengo la kutoa uelewa wa kina kwa watoto wenyewe, wazazi, walezi na jamii nzima kuhusu uwajibikaji na kulinda haki za mtoto katika ulimwengu wa mtandaoni.
Mbali na kampeni hiyo ya uhamasishaji, serikali imeanzisha rasmi Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, ambayo jukumu lake kuu ni kutoa ushauri wa kitaalamu na kusimamia mikakati thabiti ya kuzuia na kukabili vitendo vyote vya ukatili vinavyoweza kuwakabili watoto wanapotumia mifumo ya kiteknolojia.




