Breaking News

PROF. GURUMO AHIMIZA UWEKEZAJI, ELIMU NA SHERIA IMARA KUUZA UCHUMI WA BULUU

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, amesema Tanzania inahitaji kuwekeza zaidi katika elimu, teknolojia, rasilimali watu na utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha uchumi wa buluu unakuwa endelevu na unatoa manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Profesa Gurumo amesema pamoja na kuongeza matumizi ya rasilimali za bahari kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi, ni muhimu kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa na kutunzwa ili zisiishie kutokana na matumizi yasiyo endelevu.

Amesema kongamano hilo limeonesha kuwa fursa nyingi za uwekezaji na ujasiriamali katika uchumi wa buluu bado zinahitaji uwezeshaji wa kifedha, hivyo taasisi za fedha zinapaswa kubuni mifumo itakayowawezesha wajasiriamali kupata mitaji na kukuza shughuli zao.

“Tunatambua kwamba tunatazama matumizi bora ya maji tuliyonayo na rasilimali zake kwa faida za kiuchumi, lakini tusije tukajisahau kwamba tusipozitunza rasilimali hizi zinaweza kufikia mwisho na kuisha,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Gurumo, ushirikishwaji wa jamii ni miongoni mwa misingi muhimu ya uchumi wa buluu, hivyo wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka bahari na vyanzo vingine vya maji wanapaswa kupewa elimu kuhusu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia kwa njia endelevu.

Amesema pia Tanzania inapaswa kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani, hususan katika taasisi za elimu na mafunzo zinazozalisha wataalamu wa sekta ya bahari.

“Tunahitaji kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kutoa vijana ambao wanaenda kazini wakielewa wanachokifanya, lakini pia industry iweze kufaidika,” amesema.

Akizungumzia sheria na sera, Profesa Gurumo amesema kongamano hilo limebaini umuhimu wa kuhakikisha mikataba na sheria za kimataifa zinazohusu bahari zinaridhiwa na kutekelezwa kikamilifu, sambamba na kuweka sheria na miongozo ya ndani inayoiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali za bahari.

Amesema Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari (UNCLOS) ni miongoni mwa misingi muhimu inayotoa mwongozo kuhusu maeneo ya bahari, ikiwemo Territorial Sea na Exclusive Economic Zone (EEZ), pamoja na matumizi na uhifadhi wa rasilimali za bahari.

Aidha, amesema Agenda ya Afrika ya Maendeleo 2063 pia imeweka msisitizo katika matumizi ya rasilimali za bahari na uchumi wa buluu, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuongeza kasi ya kuridhia na kutekeleza mikataba na mipango inayolenga kukuza sekta hiyo.

Profesa Gurumo amesema maazimio ya kongamano hilo yameweka msisitizo mkubwa katika elimu kwa jamii na ujenzi wa rasilimali watu, akibainisha kuwa bado wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu uchumi wa buluu na fursa zake.

Amesema elimu hiyo inapaswa kuanzia ngazi za jamii, vijiji, mitaa, halmashauri na mikoa, huku wataalamu wakishirikiana na Serikali kuwafikia wananchi na kuwaeleza fursa na wajibu wao katika kulinda rasilimali za bahari.

Kwa upande wa elimu na mafunzo ya kitaalamu, amesema taasisi zinazohusika na uchumi wa buluu zinahitaji uwekezaji mkubwa katika mitambo, vifaa na teknolojia za kisasa ili wahitimu waweze kuingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta ya kimataifa.

Amesema uwekezaji huo unapaswa pia kuwahusisha wakufunzi na wataalamu, ikiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano na taasisi za elimu kutoka nchi ambazo zimepiga hatua katika sekta ya bahari.