TANZANIA YAKARIBIA KUUNGANISHWA NA SOKO LA UMEME KUSINI MWA AFRIKA
Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kuunganishwa na soko la umeme la Kusini mwa Afrika huku Mradi wa Kuunganisha Gridi za Umeme Tanzania na Zambia ukiwa umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika rasmi mnamo Februari 2027, hatua itakayoongeza uwezo wa nchi kushiriki katika biashara ya umeme kuvuka mipaka kupitia Jumuiya ya Umeme ya Kusini mwa Afrika (SAPP) na kufungua fursa za kuuza na kununua nishati hiyo kwa nchi wanachama.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 67 wa Kamati ya Usimamizi ya SAPP uliofanyika Zanzibar kuanzia Septemba 7 hadi 11, 2026, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Seif Kombo, alisema biashara ya umeme kikanda ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa nishati, kuimarisha usalama wa gridi, na kupunguza gharama za umeme, huku akisisitiza kuwa serikali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea kuwekeza katika kuimarisha miunganisho ya gridi ikiwemo mradi huo wa msongo wa kilovoti 400.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya SAPP, Andrew Etzinger, alieleza kuwa ushirikiano wa kikanda ni nguzo kuu ya kuimarisha usalama wa nishati hasa wakati huu ambapo mabadiliko ya tabianchi na ukame vinaathiri uzalishaji, akibainisha kuwa muunganisho wa Tanzania na Zambia utakuwa hatua kubwa katika kuunganisha SAPP na Jumuiya ya Biashara ya Umeme Mashariki mwa Afrika (EAPP) ili kupanua wigo wa biashara kati ya kanda hizo mbili.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usafirishaji Umeme wa Tanesco, Zakaria Mgalama, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, alieleza kuwa mkutano huo umejadili namna ya kuimarisha miundombinu na usalama wa nishati, huku akikazia kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha nafasi ya Tanzania katika mtandao mpana wa biashara ya umeme ya kikanda na kuwezesha matumizi bora ya rasilimali na miundombinu iliyopo ya uzalishaji.




