AFRIKA MASHARIKI ISHINDANE NA DUNIA, SIYO YENYEWE KWA YENYEWE - RAIS SAMIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka kipaumbele katika ushirikiano wa viwanda na kujenga minyororo ya thamani ya kikanda ili kuongeza uwezo wa eneo hilo kushindana na masoko ya kimataifa.
Akizungumza leo Alhamisi, Novemba 19, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha magari cha Double Q Motors nchini Uganda, Rais Samia amesema nchi za Afrika Mashariki hazipaswi kushindana zenyewe kwa zenyewe katika uwekezaji wa viwanda, bali zinapaswa kukamilishana na kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi imara wa pamoja.
Amesema uwepo wa kampuni zinazofanya shughuli zinazofanana katika nchi tofauti, ikiwemo Sinotrac inayopatikana Tanzania na Uganda, unaonesha umuhimu wa ushirikiano badala ya ushindani usio na tija.
Rais Samia pia amefichua kuwa Tanzania inachunguza uwezekano wa kuingia katika ushirikiano wa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza injini za treni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na mfumo na kanuni zinazofanana katika sekta ya uunganishaji na utengenezaji wa magari ili kurahisisha uwekezaji na kukuza uzalishaji wa kikanda.
Amesema lengo ni kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara badala ya kuendelea kuwa eneo linalotegemea zaidi bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.




