NESCH MINTEC YAWEKA MSISITIZO WA VIPIMO SAHIHI KATIKA BIASHARA YA MADINI
Wadau wa sekta ya madini nchini wametakiwa kutumia huduma za maabara za ndani zinazotoa vipimo vya madini kwa viwango vya kimataifa ili kupunguza gharama za utafiti, usafirishaji wa sampuli nje ya nchi na kuongeza uhakika wa matokeo ya vipimo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Nesch Mintec, Happiness Nesvinga, akieleza kuwa uwepo wa maabara hiyo jijini Mwanza utasaidia kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, hususan katika upatikanaji wa huduma za upimaji.
Amesema awali wadau wengi walilazimika kusafirisha sampuli za madini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupimwa kutokana na uhaba wa huduma hizo nchini, hali iliyokuwa ikiongeza gharama na kuchelewesha upatikanaji wa majibu ya vipimo.
Nesvinga amesema kwa sasa huduma hizo zinapatikana kupitia maabara ya Nesch Mintec iliyopo Mwanza, ambayo ina ithibati ya kimataifa (International Accreditation), inayowezesha wadau kupata huduma za vipimo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itawasaidia wadau kuokoa muda na gharama za usafirishaji wa sampuli, huku wakipata matokeo ya vipimo yenye uhakika na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za madini.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuandaa maonyesho yanayowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, akisema majukwaa hayo yanaongeza uelewa kuhusu huduma zinazopatikana nchini na kujenga mazingira bora ya uwekezaji.
Amesisitiza kuwa upimaji sahihi wa madini ni msingi muhimu wa usalama wa biashara hiyo, akiwahimiza wachimbaji na wafanyabiashara kuhakikisha wanapima madini yao ili kupata taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi, kuongeza uzalishaji na kuepuka hasara.




