MAKAMU WA RAIS MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MWAKA MMOJA OFISI YA RAIS MAENDELEO YA VIJANA
Dar es salaam - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la kitaifa la kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha pili kwenye sekta ya maendeleo ya vijana.
Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 23, 2026, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, kuanzia saa mbili asubuhi, likiwa na kaulimbiu isemayo “Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja”.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alisema maadhimisho hayo yanalenga kuutaarifu umma kuhusu mafanikio yaliyopatikana, programu zinazotekelezwa na mwelekeo wa Serikali katika kuendeleza vijana nchini.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Serikali imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kuimarisha malezi na makuzi, kutoa elimu ya uraia na uzalendo pamoja na kuratibu ushirikiano na wadau wa maendeleo ya vijana.
Nanaauka alisema kipindi hicho pia kimetumika kujenga misingi ya kuimarisha mifumo ya uratibu, ushirikishwaji na uwezeshaji wa vijana, huku vipaumbele vya utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo vikiendelea kuainishwa.
Alisema katika tukio hilo, Makamu wa Rais anatarajiwa kuzindua Mfumo wa Uwezeshaji Vijana (Youth Empowerment System – YES) na Mfumo wa Uratibu wa Maendeleo ya Vijana, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa, huduma na fursa mbalimbali kwa vijana.
Kwa mujibu wa Nanaauka, mfumo wa YES utawawezesha vijana kupata taarifa za huduma na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali, huku ukiwaunganisha na taasisi zinazotoa huduma hizo.
Alisema hadi sasa vijana 155,000 wamejisajili katika mfumo huo wakati ukiwa kwenye hatua ya majaribio, kabla ya uzinduzi wake rasmi.
Aidha, alisema Mfumo wa Uratibu wa Maendeleo ya Vijana utaweka utaratibu wa pamoja kwa wizara, taasisi za umma, serikali za mitaa na wadau wengine katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia programu za maendeleo ya vijana.
Alisema mfumo huo unatarajiwa kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na upatikanaji wa taarifa zinazohusu maendeleo ya vijana nchini.
Katika tukio hilo pia kutakuwa na maonesho ya bidhaa, huduma na ubunifu wa vijana, yatakayoshirikisha wizara za kisekta, taasisi za umma, taasisi za fedha, sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Nanauka alisema baadhi ya vijana walionufaika na programu za uwezeshaji katika kipindi cha mwaka mmoja watapata nafasi ya kueleza mafanikio yao, wakiwemo walioanzisha viwanda, mashamba makubwa ya umwagiliaji, ufugaji wa samaki kwenye vizimba na wale waliofanikiwa kupata na kutekeleza zabuni za Serikali.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yatatoa fursa kwa vijana kupata elimu na ufafanuzi kuhusu mitaji na mikopo, usajili na urasimishaji wa biashara, kodi, ununuzi wa umma, masoko na teknolojia ili kuwawezesha kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Nanaauka alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuanzisha Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, akisema hatua hiyo imeimarisha usimamizi na uratibu wa masuala ya vijana pamoja na huduma na fursa zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali.
Aliomba vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu fursa zinazopatikana kupitia programu za Serikali na wadau wa maendeleo, ili taarifa hizo ziwafikie wengi zaidi, wakiwemo wale ambao hawatahudhuria tukio hilo.




