Breaking News

RAIS SAMIA AWASILI ADDIS ABABA KUHUDHURIA MKUTANO WA AFRICA CDC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 22, 2026 amewasili jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Innocent Shiyo, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, akiambatana na Waziri wa Afya - Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, pamoja na timu kutoka Wizara ya Afya. 

Mhe. Rais Dkt. Samia amewasili nchini humo kwa ziara fupi kufuatia mwaliko kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kupambana na Magonjwa Afrika (Africa CDC), kushiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa kuhusu Afya ya Umma Afrika (CPHIA 2026), unaofanyika Novemba 23–27, 2026, ambapo anatarajiwa kuwasilisha hotuba na kuongoza mjadala wa ngazi ya juu kuhusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto barani Afrika.
Mkutano huo ni jukwaa muhimu la viongozi na wadau wa afya barani Afrika kujadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya, kukuza uzalishaji wa bidhaa tiba barani Afrika pamoja na kuimarisha utayari wa nchi kukabiliana na dharura za kiafya, kwa lengo la kujenga mifumo ya afya inayojitegemea na kupunguza utegemezi wa nje.

Tanzania imekuwa nchi inayofanya vizuri kwenye eneo la mama na mtoto chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika bara la Afrika ambapo kutokana na kazi hiyo nzuri rais ametunukiwa kuwa kinara wa Afrika katika eneo hilo.
Aidha, katika ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na taasisi ya Ibrahim, Tanzania imekuwa nchi ya nane kati ya nchi 54 za Bara la Afrika katika utoaji wa huduma bora za afya ambapo eneo la afya ya mama na mtoto ilikuwa ni miongoni mwa vigezo 7 vilivyozingatiwa.

Novemba 26 mwaka huu Mheshimiwa Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa tatu wa kitaifa wa kisayansi kuhusu afya ya uzazi,mama,mtoto mchanga,vijana na lishe utakaofanyika jijini Dar es Salaam