ULEDI: MICHANGO YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII KUPELEKWA KWA WAKATI
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu,
Bunge na Siasa, Bw. Uledi Mussa akizungumza na watumishi wa ofisi
hiyo kwenye kikao kilichofanyika mjini Dodoma leo mchana (Jumanne, Juni
21,2016). Picha na Irene Bwire wa Ofisi ya Waziri Mkuu)
Watumishi
wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu wa OWM
anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu, Bunge na Siasa, Bw. Uledi
Mussa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo
kwenye kikao kilichofanyika mjini Dodoma leo mchana (Jumanne, Juni 21,
2016). (Picha na Irene Bwire wa Ofisi ya Waziri Mkuu)
Watumishi
wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakimsikiliza Katibu Mkuu wa OWM
anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu, Bunge na Siasa, Bw. Uledi
Mussa alipokuwa akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo kwenye kikao
kilichofanyika mjini Dodoma leo mchana (Jumanne, Juni 21, 2016). (Picha na Irene Bwire wa Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………….
KATIBU MKUU Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu, Bunge na Siasa, Uledi Mussa
amesema atahakikisha michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya watumishi
wa Ofisi hiyo inafikishwa kwa wakati.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo
leo (Jumanne, 21 Juni, 2016) wakati akijibu maswali ya watumishi wa
Ofisi hiyo mjini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma
inayoanzia Juni 16 hadi 23 ya kila mwaka.
Kila mwaka Tanzania imekuwa
ikiungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya
Utumishi wa Umma Barani Afrika ambayo kauli mbiu ya mwaka huu ni
Uongozi wa Umma kwa Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.
“Nitafuatilia michango ya
watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha inafika kama
inavyotakiwa na kwa wakati ili hata wanapomaliza muda wao wa utumishi
wasihangaike,” amesema.
Katika hatua nyingine Uledi
amewataka Wakuu wa Idara kuandaa mpango wa mafunzo kwa watumishi na
washirikishe kila mtu katika idara husika kabla ya kuuwasilisha kwake.
Katibu Mkuu aliyasema hayo wakati
akijibu maswali ya baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo, ambapo Anjani
Ngulukia (Msaidizi wa Ofisi) alitaka kupatiwa ufanunuzi kuhusu suala la
michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo imekuwa haipelekwi kwa
wakati.
Pia mtumishi mwingine Ernest
Msabalala ambaye ni Mtunza Kumbukumbu Mkuu aliomba ofisi iandae
utaratibu wa kuwa na mafunzo kwa watumishi ili kuongeza ufanisi wa kazi.



