DIWANI WA ILALA ATOA WITO KWA SERIKALI KUPIGA JEKI DAR FESTIVAL
Mkurugenzi wa
kampuni ya Dar Festival, Faridi Faradji akiongea na waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu tamasha la kutangaza utamaduni wa Mtanzania mapema leo jijini
Dar es salaam, kushoto ni katibu wa kampuni hiyo Amini Kingazi.
Diwani wa Kata ya Ilala, Saady Khimji ametoa
wito kwa Serikali na Mashirika binafsi kuisaidia Kampuni ya Dar Festival ili
Iweze kufanya tamasha la kutangaza utamaduni wa nchi ya Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na
Diwani huyo ambaye pia ni Mlezi wa Kampuni hiyo alipokuwa akilitangaza rasmi
tamasha hilo mbele ya waandishi wa habari.
Khimji amesema kuwa ni jambo jema kuona
vijana wanazungumzia suala la utamaduni kwani hali hii inaonyesha dhahiri kuwa
wameamua kuirudisha nchi kwenye mstari wa kujali utamaduni wetu.
“Mataifa yote makubwa yanajali tamaduni zao
hivyo ni vema na sisi kama watanzania kuamua kwa dhati kuhakikisha tunarudisha
utamaduni wetu, jambo hili sio dogo linahitaji fedha nyingi kwahiyo, tunaomba
msaada kutoka kwa Serikali na Mashirika binafsi ili kufanikisha tamasha hili”,
alisema Khimji.
Diwani huyo ameongeza kuwa vijana hao
wamejitahidi hadi hapo walipofika lakini kama wakikosa misaada kutoka kwa
wadhamini mbalimbali basi tamasha hilo halitoweza kufanikiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo,
Faridi Faradji amesema kuwa wameamua kuisaidia Serikali kwa
kuangalia njia mbadala ya kukusanya mapato kwa kutangaza utamaduni wa Tanzania
kupitia tamasha hilo.
“Kwa namna moja au nyingine,tuna kila sababu
ya kuisaidia nchi yetu kukusanya mapato ili iweze kuendelea kwasababu baadhi ya
nchi zingine zimeweza kuendelea kupitia matamasha kama haya”, alisema
Faradji.
Naye Katibu wa Kampuni hiyo, Amini Kingazi
amesema kuwa tamasha hilo ni la asili kwahiyo wameamua kulifanyia katika ukumbi
wa Makumbusho ya Taifa kwa sababu ni eneo lenye vitu vingi vinavyoonyesha
utamaduni wa kitanzania.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kila
mwaka, Kwa mara ya kwanza litafanyika mwezi Septemba mwaka huu likijumuisha
vitu vyenye asili ya kitanzania kama vyakula vya kitanzania, mashindano ya
michezo ya kiasili pamoja na wanamuziki wa kitanzania.



