MAHAKAMA YA TANZANIA YAKUSUDIA KUBADILISHA MUONEKANO WAKE
Na Lydia Churi- Mahakama ya Tanzania
…………………………………………
Mahakama ya Tanzania imeamua
kuchukua juhudi za makusudi ili kubadilisha muonekano wake na kuwa
chombo kitakachojibu maswali na kuondoa kiu ya watanzania katika kupata
haki kwa wakati.
Akifungua Mkutano wa Mahakama ya
Tanzania na wadau wake wa kujadili utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
mhimili huo leo mjini Dodoma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya
Dodoma Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko amesema Mahakama ya Tanzania
inakusudia kukibadilisha chombo hicho ili kiweze kutoa haki kwa wakati
kwa mujibu wa jukumu ililopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Alisema katika kufanikisha azma
hiyo, Mahakama ya Tanzania inaendelea na mafunzo ya wiki mbili kwa
watumishi wake yanayolenga kuuboresha Mpango Mkakati wake kwa
kushirikiana na wadau ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati
na taswira ya mahakama inakuwa chanya wakati wote.
Jaji Kwariko amesema Mahakama
imeamua kuwashirikisha wadau kwenye Mpango Mkakati wake kwa kuwa umuhimu
na nguvu waliyonayo Sitasaidia kufanikisha utendaji wa Mahakama katika
kuyafikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Jaji Kwariko aliwataka
watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa bidii katika
kuutekeleza Mpango Mkakati kwa kuwa utendaji kazi wao utapimwa kwa jinsi
watakavyotekeleza majukumu yao kulingana na Mpango Mkakati huo.
Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania itaelekeza rasilimali zake zote kama
vile watu, fedha na muda katika kuleta matokeo makubwa yanayotarajiwa.
Alisema endapo watumishi hao
watajikita katika kufanikisha uimara wa nguzo zote tatu za Mpango
Mkakati huo, upatikanaji wa haki kwa wakati na uhusishwaji wa wadau na
imani ya wananchi vitakifanya chombo hicho kutimiza ndoto yake na
kuifikia dira yake. Nguzo tatu za Mpango Mkakati huo ni Utawala bora,
Uwajibikaji na Usimamizi wa rasilimali.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati alisema baada ya Mpango Mkakati wa
Mahakama kukamilika, watumishi watasaini kadi itakayokuwa ikionyesha
namna ya utekelezaji wa Mpango Mkakati na kadi hiyo itaweka alama za
kuonyesha ufaulu katika utekelezaji, endapo mtumishi atapata alama ndogo
atachukuliwa hatua.
Akizungumzia namna Mahakama
inavyopambana na rushwa, Msajili huyo alisema Mahakama imeweka mazingira
ya uwazi katika utoaji wa huduma zake pamoja na kuweka mifumo ya
kielekitroniki na kuhusisha wadau wake katika utendaji kazi wake.
Mahakama ya Tanzania inaendelea na
Mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake kuhusu uandaaji na utekelezaji
wa Mpango Mkakati wake ambapo leo ilikutana na wadau wake ili kujadili
namna ya utekelezaji wa Mpango huo.
Wadau waliohudhuria, mafunzo hayo
leo ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Polisi Makao Makuu, Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU na Wakala wa Majengo Tanzania-TBA.
Wengine ni pamoja na Baraza la
Habari Tanzania-MCT, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Usuluhishi wa
Migogoro, Ofisi ya Nyaraka za Taifa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-TAMISEMI.



