NMB YAORODHESHA HATI FUNGANI ZAKE KWENYE SOKO LA HISA (DSE)
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB,
Bi. Ineke Bussemaker akizungumza katika hafla ya benki hiyo kuoroshesha rasmi
hati fungani kiasi cha shilingi Bilioni 41.4 leo katika Soko la Hisa la Dar es
Salaam (DSE).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru akizungumza katika hafla ya benki hiyo
kuoroshesha rasmi hati fungani kiasi cha shilingi Bilioni 41.4 leo katika Soko
la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji – Dk. Adelhelm Meru (katikati) akipiga kengele kuashiria
kuorosheshwa rasmi hati fungani za Benki ya NMB kiasi cha shilingi Bilioni 41.4
leo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa
NMB, Bi. Ineke Bussemaker pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es
Salaam (DSE), Moremi Marwa (Kulia).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji – Dk. Adelhelm Meru (kulia) akimpongeza Mkurugenzi Mkuu
wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (kushoto) mara baada ya tukio la Benki ya
NMB kuoroshesha rasmi hati fungani kiasi cha shilingi bilioni 41.4 katika Soko
la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Na Frank wandiba;
Benki ya NMB leo imeorodhesha kiasi cha
shilingi Bilioni 41.4 ilichokipata kutokana na mauzo ya hati fungani katika
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Tukio hilo limezinduliwa rasmi leo jijini
Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk.
Adelhelm Meru kwa ishara ya kupiga kengele kwenye ofisi za DSM.
Akizungumza
katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji – Dk.
Meru amepongeza hatua hiyo ya kuorodhesha hati fungani kwenye soko la hisa na
kuongeza kuwa ni ya kizalendo na kuwataka wawekezaji katika sekta binafsi
kushiriki kikamilifu.
“Hati fungani hii
inatarajiwa kuleta maendeleo katika soko la mitaji na inafungua njia kwa
mashirika mengine binafsi, mashirika ya serikali na mamlaka za manispaa
kutafuta njia mpya za kukuza mitaji na uwezeshaji” alisema Dk. Adelhelm.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa NMB – Ineke Bussemaker alisema “Hati fungani hii ya miaka
mitatu si tu imeleta msisimko chanya kwenye soko la mitaji bali hata katika
soko la hisa, NMB inakuwa benki ya kwanza kupata Kiwango zaidi ya mara mbili ya
Kiwango tulichoomba awali.”
Bi Ineke
aliongeza kuwa mwitikio chanya kwenye hati fungani ya NMB unatoa somo kuwa kuna
umuhimu wa benki mbalimbali kuchangia kwa Kiwango kikubwa katika kuendeleza
masoko ya mitaji na pia kupigania elimu ya fedha kwa jamii.
Hati fungani
inayoorodheshwa leo ina riba ya asilimia 13 kwa mwaka na iitakomaa baada ya
miaka miatatu.
Bi Ineke alisema
Kutolewa kwa hati fungani ya NMB ni sehemu ya mkakati wa benki kutafuta njia
mbadala za vyanzo vya fedha. Fedha zilizopatikana kwenye hati fungani
zitatumika kwaajili ya kutoa mikopo kwa wateja, wateja watakaonufaika ni pamoja
na wateja binafsi, wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa pamoja na taasisi
za serikali.
Akiongea kwenye
hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE – Moremi Marwa alisema “mafanikio ya
Hati fungani ya NMB yanatuambia kuwa wawekezaji wanajua uwepo wa fursa zilizopo
katika masoko ya mitaji na wana uwezo na hamu ya kusaidia wale walio na uhitaji
wa kukuza mitaji yao.”
Hati fungani ya
NMB ilipata mwitikio chanya kutoka kwa wawekezaji na kupita Kiwango
kilichopangwa awali kwa asilimia 107. Benki ilipata maombi 1,811 yenye thamani
ya shilingi bilioni 41.4 huku maombi mengi yakirundikana wiki ya mwisho kabla
ya kufunga upokeaji wa maombi.
Kutokana na kuorodheshwa kwenye soko la hisa,
wawekezaji wataweza kuuza hati fungani zao kupitia soko la hisa la Dar es
Salaam – DSE.
Stanbic Bank
Tanzania Ltd. Ndio wawezeshaji wa hati fungani ya NMB huku makampuni ya Orbit
Securities Ltd. na EA Capital Ltd wakiwa kama mawakala viongozi.







