SAKATA LA KUFUNGIWA TABIBU DK MWAKA LACHUKUA SURA MPYA.
HATUA iliyochukuliwa ya kufungia kituo cha tiba asili cha tabibu Dk. Juma Mwaka ‘Foreplan’ pamoja na vituo vingine viwili, kumesukumwa na maslahi binafsi,
Na; Regina Mkonde.
“Baraza la Tiba Asili
na Tiba Mbadala nchini limelalamikiwa kuchukuwa hatua hiyo kutokana na kuwepo
kwa msukumo wa binafsi ya baadhi ya watumishi wa baraza hilo na kwamba, sababu
zilizotolewa ni za ‘kipuuzi”
Amesema , hatua hiyo ni juhudi za
kurudisha nyuma ama kukwamisha kwa makusudi juhudi za waganga wa Tiba Asili.
Hayo yamesemwa leo na Mohamed
Matokeo, Mwenyekiti wa Baraza la Waganga wa Tiba, Ushauri na Utafiti wa Dawa
Asili Tanzania (Bawata) wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam.
“Bawata tukiwa chombo huru cha
waganga wa tiba asili, tunasikitika sana utendaji kazi unaofanywa na Baraza la
Tiba Asili na Tiba Mbadala ambacho ni chombo cha kiserikali kilichopewa mamlaka
ya kusimamia taaluma hii na kuiendeleza,” amesema na kuongeza;
“Lakini baraza hilo limekuwa ni
chombo kinachorudisha nyuma fani ya tiba asili hapa nchini, kwani limekuwa
likikwamisha kwa makusudi juhudi za waganga wa tiba asili walioonesha ufanisi
katika kutoa huduma ya tiba asili.
Imekuwa kawaida kwa baraza hilo
kuitisha au kuwafungia waganga wa tiba asili na vituo vyao kwa sababu
zinazoonekana ni za kibinafsi.”
Matokeo ametoa mfano wa tukio
lililotokea jana la kufungwa kwa baadhi ya vituo vya tiba asili ambapo amesema
kuwa, wahusika walifungiwa pasipo kupewa nafasi ya kujitetea na au kuhojiwa.
“Sisi bawata tunapinga hatua hii ya
kiuonevu kwani wametoa maamuzi ya kuwafungia bila ya kuwahoji wahusika, tena
hawa ni waganga halali kisheria wamesajiliwa na wanalipa kodi vizuri,” amesema.
Sharifu Karama, Katibu Mkuu Taifa wa
Bawata amedai kuwa, kuna baadhi ya watumishi wa afya wanaojishughulisha na
uuzaji wa dawa za tiba asili kwamba ndiyo wanaochochea kukandamizwa kwa
masilahi ya waganga wa tiba asili nchini.
“Kuna baadhi ya watumishi wa afya
wanauza dawa za tiba asili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo
kwenye jengo la serikali.
“Kutokana na hali hiyo, Bawata
tunaamini kwamba, baraza la tiba asili na tiba mbadala linaongozwa na waganga
wa kisasa na kwamba tuna taarifa kuwa, kuna baadhi ya viongozi wa baraza hilo
nao wanauza dawa asili kwa hiyo wanalitumia baraza kutimiza hadhma yao,”
amesema.
Hata hivyo, Foreplan ilianza
kuwindwa na Hamis Kigwangala, Naibu Waziri wa Afya baada ya kufanya ziara ya
kushtukiza tarehe 15 Desemba mwaka jana na kuibua maswali mengi.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa
kutolewa siku saba za uchunguzi na kwamba, kinachofanyika sasa kinatajwa kuwa
ni matokeo ya ‘dhamira’ iliyooneshwa baada ya ziara hiyo.



