Kauli Ya Katibu Wa Chadema Mkoa Kilimanjaro..kufatia Mbunge Mwingine Wa CHADEMA Kujiuzulu Na Kuhamia CCM

Barua na video iliyosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii ikieleza mbunge wa Siha (Chadema) mkoani Kilimanjaro, Dk
Godwin Mollel amejiuzulu ubunge imezua mjadala.
Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro,
Basil Lema leo Alhamisi Desemba 14,2017 amesema naye ameona video na barua
kwenye mitandao ya kijamii lakini hawana uthibitisho wowote.
"Mheshimiwa Mollel hakuwahi
kuonyesha dalili yoyote kuwa yuko kwenye hilo wimbi na mimi nimeona hiyo barua
na video kwenye mitandao. Bado kwangu nachukulia kama uvumi mpaka
tutakapothibitisha," amesema.
Lema amesema kwa utaratibu alipaswa
kumuandikia barua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe au
viongozi wa Chadema.
Amesema akiwa katibu wa mkoa wa chama
hicho hajapokea barua yoyote kutoka kwa Dk Mollel.
"Ukiangalia hata barua
inayosambaa haijasainiwa na video inaonyesha ni mtu tu kajirekodi akarusha.
Katika mazingira hayo hatuwezi kukurupuka kuzungumzia hilo jambo,"
amesema.
Taarifa inayosambaa kwenye mitandao
ambayo haina saini inaonyesha kuandikwa na Dk Mollel akieleza ameamua kujivua
uanachama wa Chadema kuanzia leo Alhamisi Desemba 14,2017.
Pia, ametangaza kujiuzulu nafasi ya
ubunge na kwamba huo ni uamuzi wake alioufanya akiwa na akili timamu na
hajashinikizwa na mtu yeyote.



