Makamu Wa Rais Ahamia Rasmi Dodoma
Na Beatrice Lyimo, MAELEZO-DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan amehamia rasmi Makao Makuu ya Nchi Dodoma leo ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alililitoa tarehe 25, June.
“Siku ya leo ilikuwa mawazoni mwangu, ninafurahi imefika na pia
ninamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa maandalizi mazuri ya kunipokea ” Alisisitiza
Mhe. Samia
Aidha, Mhe. Samia amesema kuwa Ofisi yake imekuja na agenda ya
kuifanya Dodoma kuwa ya kijani hivyo wameandaa programu mbalimbali ikiwemo
ya upandaji miti .
“Tarehe 21, Disemba mwaka huu kutakuwa na shughuli ya upandaji
miti hivyo tunaomba wakazi wa mkoa wa Dodoma kutuunga mkono ili kuweza kutimiza
azma hii” ameongeza Mhe. Samia.
“Tunaendelea kuamini kwamba tamko la Rais linatekelezeka ambapo
mpaka sasa watumishi 2816 tayari wameshahamia Dodoma na wanaendelea kutoa
huduma za Serikali na kuanzia Februari mwaka 2018 tunaendelea
kupokea watumishi wengine” amefafanua Waziri Mkuu.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma
Pancras Ndejembi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutimiza historia ya
Mwalimu Nyerere ya Dodoma kuwa Makao Makuu.
Kwa upande wake Balozi Job Lusinde amesema kuwa “leo Makamu wa
Rais anahamia Dodoma, kweli Mungu hupanga na Mungu huweka wakati wake, leo
imekuwa”.
Mbali na hayo Balozi Job Lusinde amesema kuwa Makamu wa Rais amekuja kipindi ambacho Mkoa wa Dodoma unaanza kuandaa mashamba kwa ajili ya
kulima, hivyo kumpatia jina la kabila hilo “Mbeleje” likimaanisha kipindi cha kuandaa mashamba.



