RAIS MAGUFULI AITAKA KAMPUNI YA TOTAL KUHARAKISHA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na viongozi wa kampuni ya
Total ambayo ni mwekezaji mkubwa wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la
kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania na
kuwahakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo na
washirika wengine katika ujenzi wa mradi huo.
Viongozi wa Total waliokutana na Mhe.
Rais Magufuli jana tarehe 05 Desemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es
Salaam ni Rais wa masoko na huduma Bw. Momar Nguer, Rais wa Total Afrika Bw.
Stanislas Mittelman, Makamu wa Rais wa Total wa Afrika ya Kati na Afrika
Mashariki Bw. Jean Christian Bergeron na Mkurugenzi Mtendaji Total Tanzania Bw.
Tarik Moufaddal.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Total
kuharakisha ujenzi wa bomba hilo uliopangwa kuanza mwezi ujao na kukamilisha
mapema hata kabla ya mwaka 2020 uliopangwa ili wananchi wa Tanzania na Uganda
waanze kunufaika na mafuta hayo.
“Tuna matumaini makubwa na Total kuwa
kazi hii mtaifanya haraka, na naomba niwahakikishie kuwa pamoja na soko la nje,
kuna soko kubwa Afrika Mashariki yenye watu Milioni 165, na Serikali ya
Tanzania itawapa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa ujenzi na uendeshaji wa
mradi ili mradi mnalipa kodi vizuri na mnazingatia sheria zetu” amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka
kampuni hiyo kuzingatia kutoa ajira kwa Watanzania katika wilaya 24 ambazo
bomba litapita huku akiwahakikishia kuwa Tanzania inao wakandarasi na wahandisi
wa kutosha na wenye uwezo wa kushirikiana nao katika ujenzi wa bomba hilo.
Baada ya mazungumzo hayo Waziri wa
Nishati Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw.
Charles Mwijage wamesema pamoja na kuja nchini kuangalia maandalizi ya ujenzi
wa bomba, viongozi wa Total wameamua kuimarisha soko la mafuta Tanzania na pia
kushirikiana na Serikali katika utafiti wa mafuta katika maeneo ya Ziwa
Tanganyika, Eyasi Wembere na Ziwa Rukwa.
Kwa upande wake Bw. Momar Nguer
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta
Museveni kwa msukumo mkubwa walioutoa katika kufanikisha mradi huu na ameahidi
kuwa Total itahakikisha inakamilisha haraka mambo machache yaliyobaki ili
kuanza ujenzi bila kuchelewa.
Bw. Momar Nguer amempongeza Mhe. Rais
Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na rushwa jambo lililosaidia kuimarisha
mazingira ya uwekezaji na amemuhakikishia kuwa Total ipo tayari kufanya kazi
bega kwa bega na Tanzania katika jukumu la utafiti wa mafuta katika maeneo yote
yaliyotajwa.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli
ameagana na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) aliyemaliza muda wake
Mhe. Abdulla Ibrahim Alsiwaidi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe.
Abdulla Ibrahim Alsiwaidi kwa utumishi wake wa miaka 5 na amemuomba amfikishie
salamu za shukrani kwa Rais wa UAE Mtukufu Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan
kwa ushirikiano ambao Tanzania inaupata katika Nyanja mbalimbali za maendeleo
na ustawi wa jamii.



